Serikali imeuagiza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kuweka kizuizi kupitia Mfumo wa TEHAMA, kitakachozuia mwanachama wa Mfuko huo kutoka Hospitali ya ngazi ya juu kwenda kupata huduma ngazi ya chini.

Zuio hilo linalenga kudhibiti udanganyifu na kuzingatia taratibu za huduma za matibabu ambazo zinamhitaji mgonjwa kutoka ngazi ya chini kwenda ngazi ya juu.

Agizo hilo lilitolewa juzi na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa kikao kati ya NHIF na Watoa huduma wa Mkoa wa Dar es Salaam ambacho kililenga kuweka mikakati ya pamoja ya uboreshaji wa huduma za matibabu kwa wananchi na wanachama wa Mfuko.

"Hili natoa agizo wekeni kizuizi ambacho Mwanachama hatahamishwa kutoka Hospitali ngazi za juu mfano Muhimbili, MOI na Hospitali za Kanda na kushushwa kwenye ngazi za chini, huu ni uchochoro wa udanganyifu na matumizi yasiyo sahihi ya huduma za NHIF," alisema Mhe. Ummy.

Mbali na hilo, alisema kuwa Serikali pia itaangalia namna ya kuwepo kwa Mdhibiti wa Huduma za Bima ya Afya ambaye atashughulikia masuala ya bei za huduma za matibabu ili kuepukana na upandaji wa gharama kiholela. 

"Nakubaliana kabisa na suala la kuwepo kwa Mdhibiti ili tuwe na bei halisia lakini pia Tume ya Usuluhishi kati ya Mtoa Huduma, Mwanachama na NHIF ili kusuluhisha migogoro inayoweza kujitokeza baina yao " alisema Mhe. Waziri.

Kwa upande wake Mkurugenzi  Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga, alisema kuwa NHIF umelichukua kwa utekelezaji agizo la kuweka kizuizi cha mwanachama kuhamishwa kutoka ngazi za juu kwenda chini Hospitali.

Akizungumzia suala la Tume ya Usuluhishi alisema Mfuko uko tayari kwa hilo kwa kuwa ndio muathirika mkubwa hasa katika masuala ya udanganyifu ambayo yanatishia uhai wa Mfuko.

"NHIF inamhitaji zaidi huyu Mdhibiti ili turejee kwenye bei halisi na Tume ya Usuluhishi nayo itatusaidia sana sisi kumaliza malalamiko ya kukatwa fedha kwa Watoa huduma hasa zinazotokana na udanganyifu ," alisema Bw. Konga.

Akizungumzia wigo wa wanachama alisema kuwa hadi Machi mwaka huu Mfuko unahudumia jumla ya wanufaika 4,639,000 na jumla ya vituo vilivyosajiliwa ni 8,883.

Aidha Bw. Konga alisema kuwa ili Mfuko uendelee kuwa imara una mikakati mbalimbali ikiwemo kusajili wananchi wengi zaidi kwa makundi mfano wanafunzi hoja ambayo Mhe. Ummy alikubaliana nayo na akasema Serikali inafanya kila jitihada kulinda uhai wa Mfuko kutokana na ukweli kwamba vituo vyote havina uwezo wa kujiendesha bila kuwa na NHIF.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...