Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
MTANDAO wa Vijana wanaoishi na Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (NYP+) wameiomba Serikali, Mashirika na Wadau mbalimbali nchini kushikamana nao ili kuondokana na kutokomeza maambukizi mapya ya Virusi hivyo ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza na Michuzi Blog jijini Dar es Salaam, Mwakilishi wa Mtandao huo, Cyprian Komba amesema Vijana hao wanahitaji rasilimali mbalimbali ili kuwawezesha kufika sehemu mbalimbali na kutoa elimu ili kufikia malengo yao sanjari na kujenga Uchumi imara wa taifa na Uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Komba amesema ili kuondokana na hali ya unyanyapaa kwa watu wanaoishi na maambukizi ya VVU, Jamii inapaswa kupewa elimu ya kutosha kuhusu maambukizi hayo licha ya takwimu za Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) kueleza kuwa kwa kiasi kikubwa unyanyapaa umepungua sehemu mbalimbali nchini.
“Tunahitaji kuwezeshwa na Serikali, wadau mbalimbali ili tuweze kutoa elimu kwa jamii yetu na kuondokana na fikra potofu juu ya maambukizi ya VVU, pia tuondokane na unyanyapaa ili kila mmoja achangie kujenga Uchumi imara wa nchi”, amesema Komba.
“Hali ya unyanyapaa kwa mtu mmoja mmoja bado ipo, Mfano, Mtu mmoja alikuwa anafanya biashara ya ‘Saloon’ kutokana na mazingira hayo, watu walivyojua yeye ana maambukizi walimnyanyapaa licha ya yeye kutumia Dawa za kufubaza Virusi hivyo”, ameeleza Komba
Pia, ametoa mwito kwa Vijana hao ambao ni wahusika zaidi, kusimama kidete na kuwa mstari wa mbele kupiga vita unyanyapaa, pia kuelewa mambo kwa upana wake na kutokomeza hali hiyo ya unyanyapaa kwa baadhi ya watu wenye imani potofu.
Naye, Mshiriki wa Mdahalo huo, Emiliana Kimario amesema watatumia midahalo hiyo kupeleka ujumbe kwa Jamii mbalimbali ili kujitambua wao kama Vijana, pia kutoa elimu kuhusu maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutokana na wao kuwa walengwa wakubwa wa maambukizi hayo.
Kupitia mdahalo huo kati ya Vijana wanaounda Mtandao huo, Viongozi wa Dini na wadau mbalimbali, Sheikh wa Msikiti wa Noor - Mbezi Beach, Mzamil Rajab ametoa mwito kwa Vijana kuhakikisha wanajali Afya zao katika umri wao wa ujana sanjari na kuepuka anasa zisizokuwa za msingi na kumkumbuka Mwenyezi Mungu.
“Katika vitabu vya dini ya Kiislamu, Mtume Mohammad (S.W.A) ameeleza “enyi vijana, ambao mmefika umri wa kuoa oeni”, maneno haya yamesemwa ili kumuepusha Kijana na anasa na kumuepusha kijana na adhabu ya maradhi yaliyotanda ulimwenguni”, amesema Sheikh.
Mwakilishi wa Mtandao wa Vijana wanaoishi na Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (NYP+), Cyprian Komba akizungumza na Vijana wanaounda Mtandao huo wakati wa mdahalo baina yao, Viongozi wa Dini, Serikali na Wadau mbalimbali.
Sheikh wa Msikiti wa Noor - Mbezi Beach, Mzamil Rajab akitoa darasa kwa vijana wanaounda Mtandao wa Vijana wanaoishi na Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (NYP+) wakati wa mdahalo baina ya Vijana hao, Viongozi wa Dini, Serikali na Wadau mbalimbali katika Siku ya Vijana.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...