
Wafanyakazi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) akiwa na Kombe mara baada ya kuibuka washindi wa kwanza taasisi za serikali katika masuala ya Chakula, ushauri na Katika Maonesho ya Chakula yaliyofanyika Mkoani Simiyu.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Wafanyakazi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) wakiwa katika picha ya pamoja katika maonesho ya Chakula Mkoani Simiyu.
WAKALA wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula – NFRA ni taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Kilimo iliyoanzishwa kwa sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 ya mwaka 1997 na ulianza kazi rasmi tarehe 1 Julai, 2008.
Jukumu kuu la NFRA ni kuihakikishia nchi usalama wa chakula kwa kununua na kuhifadhi akiba ya chakula na kutoa chakula cha msaada kwa waathirika waliokumbwa na majanga mbalimbali ya Kitaifa. Aidha, Wakala huzungusha akiba ya chakula kwa lengo la kutoa nafasi ya uhifadhi na kuingiza mapato ya kununua akiba mpya ya chakula. Mazao yanayonunuliwa na kuhifadhiwa kwa sasa ni mahindi, mtama na mpunga.
NFRA hutekeleza majukumu yake nchi nzima kupitia kanda nane ambazo ni Arusha, Dodoma, Kipawa, Shinyanga, Songea, Songwe, Makambako na Sumbawanga. Kwa sasa, NFRA ina uwezo wa kuhifadhi tani 341,000 kwa kutumia maghala na vihenge vya kisasa.
MAJUKUMU YA WAKALA
Majukumu ya msingi ya Wakala ni haya yafuatayo;
i. Kununua na Kuhifadhi Nafaka: Wakala hununua nafaka kutoka katika maeneo yaliyozalisha ziada ya chakula hususan vijijini kuanzia mwezi Julai. Ununuzi hufanyika kupitia vituo vya ununuzi vya Wakala na vikundi/vyama vya wakulima. Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Wakala umepanga kununua tani 100,000 za nafaka.
ii. Kukabiliana na Upungufu wa Chakula: Wakala una wajibu wa kutoa chakula kwa walioathirika na upungufu wa chakula kutokana na majanga mbalimbali kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na Serikali. Chakula hicho hutolewa kwa kuzingatia matokeo ya tathmini ya hali ya chakula nchini inayofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau wengine. Aidha, chakula hicho hutolewa kwa Halmashauri husika baada ya kuidhinishwa na Kamati ya Kuratibu Maafa nchini chini Ofisi ya Waziri Mkuu.
iii. Kuzungusha Akiba ya Chakula: Kwa utaratibu uliojiwekea, Wakala huzungusha sehemu ya akiba ya chakula kwa kuuza kwa lengo la kuhakikisha kuwa chakula kinachohifadhiwa hakiharibiki, kupata nafasi ya uhifadhi katika maghala na kupata fedha za ununuzi wa akiba mpya. Chakula hicho huweza kuuzwa kwa wadau mbali mbali ndani na nje ya nchi. Kwa mwaka wa Fedha 2022/2023, Wakala umepanga kuzungusha takriban tani 124,000 za nafaka.
Aidha, mbali na majukumu haya ya msingi Wakala unatekeleza majukumu mengine miongoni mwake yakiwa ni kutoa elimu kwa Wadau kuhusu uhifadhi bora wa nafaka,kuchochea soko la nafaka nchini na kupunguza mfumuko wa bei za nafaka.
MAFANIKIO
Wakala umepata mafanikio makubwa katika Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imekuwa ni nguzo imara ya kuongeza ufanisi wa NFRA katika utekelezaji wa majukumu yake. Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni haya yafuatayo;
i. Kuongezeka kwa ununuzi wa Akiba ya chakula: Serikali ya Awamu ya Sita imewezesha Wakala kuongeza uwezo wa kununua akiba ya kutosha ya chakula kila mwaka. Kumekuwa na ongezeko la ununuzi kutoka takriban tani 58,000 kufikia zaidi ya tani 110,000 za nafaka kwa mwaka 2021/2022. Ununuzi wa nafaka kwa msimu wa mwaka 2022/2023 unaendelea kupitia kanda za Sumbawanga (mikoa ya Rukwa na Katavi), Songea (mkoa wa Ruvuma), Arusha (mkoa wa Manyara), Shinyanga (mkoa wa Kigoma), Makambako (mikoa ya Iringa na Njombe), Songwe (mikoa ya Songwe na Mbeya) na Dodoma.
ii. Kuongezeka kwa Akiba ya Chakula: Serikali ya awamu ya Sita imeimarisha hifadhi ya chakula nchini kwa kuongeza akiba ya chakula inayohifadhiwa na Wakala kuwa zaidi ya mara mbili ya kiasi kilichokuwa kinahifadhi kipindi cha miaka mitatu ya hivi karibuni. Ongezeko la hifadhi ya chakula imewezesha Wakala kuwa na akiba ya kutosha ya chakula kwa ajili ya kuhudumia kwa wakati mahitaji mbalimbali ya dharura au upungufu wa chakula unaoweza kujitokeza nchini.
iii. Kupunguza kasi ya mfumuko wa bei za nafaka: Kama ilivyoelezwa awali na Mhe. Waziri wa Kilimo kwamba nchi kwa ujumla ina utoshelevu wa chakula. Kwa baadhi ya maeneo yenye kasi kubwa ya kupanda kwa bei za nafaka, kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Wakala umefanikiwa kukabiliana na makali ya mfumuko wa bei za nafaka katika maeneo yaliyohudumiwa, kwa lengo la kupunguza makali kwa kuongeza upatikanaji wa nafaka katika masoko hivyo kuleta unafuu katika maisha ya wananchi. Kwa kuanzia, Wakala unahudumia Halmashauri za Bunda, Sengerema, Geita, Nzega, Liwale, Nachingwea, Longido, Loliondo na Monduli ambapo takriban tani 3,000 zimepelekwa katika maeneo hayo. Wakala kwa niaba ya Serikali umejipanga kuhudumia halmashauri nyingine zinazoweza kuthibitika kuwa na upungufu wa chakula ili kuleta unafuu kwa wananchi.
iv. Kukamilisha sehemu ya mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka (vihenge na maghala): Wakala unatekeleza Mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka ambapo mradi huo ukikamilika utaongeza uwezo wa kuhifadhi kutoka tani 251,000 hadi tani 501,000. Kwa sasa NFRA ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, Wakala umefanikiwa kukamilisha sehemu ya Mradi na kuongeza uwezo wa kuhifadhi kwa tani 90,000 katika Kanda za Arusha (Halmashauri ya Babati) na Sumbawanga (Sumbawanga na Mpanda). Kukamilika kwa mradi huo kumeongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka kutoka tani 251,000 hadi tani 341,000. Utekelezaji wa Mradi katika maeneo mengine Dodoma, Songea, Shinyanga, Songwe na Makambako umefikia asilimia 85.
v. Kuwa soko la uhakika la wakulima: Serikali ya Awamu ya Sita imewezesha NFRA kuimarisha uchumi wa makundi mbalimbali yakiwamo ya Wakulima, vyama vya ushirika, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla kupitia mapato yanayopatikana kwa kuuza nafaka kwa NFRA, hivyo kuwa soko la uhakika kwa wakulima. Wakala umekuwa ukinunua nafaka kwa bei nzuri hivyo kuwa soko tegemezi kwa wakulima wengi na kuwapo motisha wakulima kujishughulisha na Kilimo.
vi. Kuchangia mapato ya Halmashauri na Serikali Kuu: Utekelezaji jukumu la ununuzi, uhifadhi na uzungushaji wa akiba ya chakula unachangia mapato kupitia malipo ya ushuru wa mazao (crop Cess) wakati wa ununuzi/mauzo ya nafaka na ukusanyaji wa kodi ya zuio (Withholding Tax) kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
vii. Kutoa ajira kwa wananchi na Sekta Binafsi: NFRA imefanikiwa kuongeza fursa za kiuchumi kwa sekta mbalimbali kupitia kazi za usafirishaji, ununuzi wa vifaa mbalimbali vya uhifadhi na viuatilifu. Aidha, NFRA hutoa kutoa ajira za muda mfupi kwa wananchi zaidi ya 3,000 zinazochangia kuongeza kipato kwa wananchi. Ajira hizo zinazotokana na kazi mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa zoezi la ununuzi wa nafaka, uhifadhi na kipindi cha uzungushaji wa nafaka na utekelezaji wa Mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka.
viii. Kutoa elimu kwa Wadau kupitia matukio mbalimbali: Wakala umekuwa ukitoa elimu katika masuala ya uhifadhi kwa Wananchi mbalimbali kupitia njia mbalimbali ikiwamo vyombo vya habari na matukio ya Kitaifa na Kimataifa
MIKAKATI
Ili kuendelea kuihakikishia nchi usalama wa chakula, Wakala una mikakati ya kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka, kukamilisha Mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka unaoendelea kutekelezwa, kuboresha miundombinu ya uhifadhi, kuendelea kutoa elimu kwa wadau kuhusu uhifadhi bora wa nafaka, kuimarisha mifumo ya kiutendaji na kujengea uwezo watumishi katika nyanja mbalimbali.
Wakala umejipanga kuhudumia maeneo mengine yatakayothibitika kuwa na mahitaji ya dharura au upungufu wa chakula. Aidha, Wakala unatoa wito kwa wananchi wote kwamba, ili kujihakikishia usalama wa chakula kuanzia ngazi ya kaya, wahifadhi akiba ya kutosha ya chakula kipindi cha mavuno na kuuza chakula pale wanapokuwa na ziada katika uzalishaji.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...