Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha wanakuja na mpango madhubuti utakaoweza kukuza lugha ya kiswahili ndani na nje ya nchi.

Ili kufanikisha hilo, ameitaka wizara hiyo kuhakikisha  bidhaa zote zinazozalishwa katika viwanda vya hapa nyumbani na zile zinazoingizwa kutoka nje ya  nchi, zinakuwa na maelezo yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili ili watumiaji wa bidhaa hizo wazitumie wakiwa wanafahamu vyema maelekezo yaliyomo kwenye bidhaa.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Januari 25, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kutoa Tuzo ya Kiswahili ya Safal-corneal ya Fasihi ya Afrika iliyoandaliwa na Kampuni ya Mabati ya Alaf Tanzania, hafla ya Tuzo hizo zimefanya katika Ukumbi wa Mlimani City.

Pia, amezitaka Mamlaka husika zisimamia kuhakikisha Lugha ya Kiswahili inatumika katika maeneo mbalimbali ikiwemo; maelekezo ya dawa hospitali, matangazo, alama za barabarani na majina ya shule, hoteli na mengineyo 

Aidha Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo yenye dhamana ya lugha ya Kiswahili, kuanzisha tuzo maalumu ya Kazi za Kiswahili katika Sayansi na kuendelea kuratibu vema na kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha lugha ya Kiswahili inakua, kuenea na Tanzania kuendelea kuwa kinara wa maendeleo ya lugha hiyo.

Waziri Mkuu pia ameziagiza mamlaka husika kuzingatia maelekezo yanayotolewa na viongozi waandamizi kwa nyakati tofauti kuhusu kueneza lugha hiyo na kuanzisha mpango mkakati wa utekelezaji wake.
Amesema, Julai 7, 2022 wakati wa maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Kiswahili Duniani, Makami wa Rais Dk Philip Mpango, alitoa maagizo ambayo yanahitaji hatua za utekelezaji hivyo amewataka kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa kikamilifu.

Aidha ametoa wito kwa asasi zinazohusika na maelekezo aliyoyatoa Dkt. Mpango na aliyoyatoa leo kufanya tathmini ya utekelezaji ili  kuyaripoti katika maadhimisho yajayo ya Siku ya Kiswahili.

Aidha, ameigiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuandaa mitaala mipya ya elimu itakayosaidia kukuza kiswahili kwa kuyashirikisha makundi mbalimbali ikiwemo wanawake na vijana.

Akiendelea kuzungumza katika hafla hiyo Waziri Mkuu huyo ametoa msisitizo wa mambo matatu ya kuzingatiwa katika ukuzaji na uenezaji wa Kiswahili na kuagiza kuwe na mkakati wa kutangaza Kiswahili ndani na nje ya nchi kwa kuandika na kusambaza kamusi na vitabu vya Kiswahili vitakavyowasaidia watu kujifunza lugha hiyo adhimu.

"Wataalamu wa Kiswahili hakikisheni mnaweka mikakati thabiti ya kupenyeza Kiswahili nje ya nchi kwa njia mbalimbali…  Vilevile, sambazeni vijitabu vyenye misamiati muhimu kwa wasomaji wa awali wa lugha ya Kiswahili, viwekeni kwenye mitandao ili viweze kusomwa na watu wengi zaidi duniani,” ameeleza.
Alihimiza Kiswahili kutumika katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja huduma za jamii, mikutano, warsha na makongamano; na kuagiza tafiti za lugha ya Kiswahili kuimarishwa.

Naye, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohammed Mchengerewa amesema Kiswahili ndio lugha kuu nchini inayowaunganisha watanzania wenye makabila zaidi ya 150 na kwamba  kwa sasa lugha hiyo inaenea kwa kasi ikiwa ni moja kati ya lugha 10 mashuhuri duniani. 

Mchengerwa amesema, hatua hiyo bado haitoshi, kasi ya usambazaji wake haijakua ikiwemo fursa nyingi za lugha hiyo nje ya mipaka ya Tanzania ambazo bado hazijatumiwa vizuri hivyo bado kuna kazi kubwa ili kuhakikisha lugha ya kiswahili inazidi kupaa ulimwenguni kote.

Kwa upande wake, amesema, Mkurugenzi Mkuu wa Alaf Tanzania Ashish Mistry alisema amesema, kampuni ya Alaf imekuwa ikidhamini tuzo hizo kwa muda mrefu tangu zianzishwe mwaka 2015 na sasa imeongeza udhamini wake ambapo sasa wanafunzi wa shahada ya umahiri ya Kiswahili kupitia chuo kikuu cha Dar es salaam takribani 12 wamepata ufadhili huo.

Washindi wa tuzo hizo waliobuka kinara wote ni Watanzania. Mshindi wa kwanza kwa upande wa riwaya ni  Doto Rangimoto na mshindi wa kwanza katika ushairi ni Salum Makamba ambao wote wamejinyakulia dola za Marekani 5,000 sawa na Sh milioni 11.6.

Mshindi wa pili katika riwaya ni Isaac Ndolo na wa pili katika ushairi ni Ally Mchanyato ambao wote wamejinyakulia dola za Marekani 2,500 sawa na Sh milioni 5.8.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi tuzo pamoja na hundi ya Dola 5,000, mshindi wa kwanza wa Riwaya, Dotto Daudi, kwenye hafla ya utoaji Tuzo ya Kiswahili ya Safal – Cornell ya Fasihi ya Afrika mwaka 2022, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani, jijini Dar es salaam Januari 19, 2023. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkuu – ALAF Tanzania, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammed Mchengerwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makala. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukabidhi Tuzo ya Kiswahili ya Safal – Cornell ya Fasihi ya Afrika mwaka 2022, kwenye Ukumbi wa Mlimani, jijini Dar es salaam Januari 19, 2023.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammed Mchengerwa, akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi Tuzo ya Kiswahili ya Safal – Cornell ya Fasihi ya Afrika mwaka 2022, katika Ukumbi wa Mlimani, jijini Dar es salaam Januari 19, 2023.
 Mkurugenzi Mkuu SAFAL Group Anders Lindgren, Ashish Mistry  akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi Tuzo ya Kiswahili ya Safal – Cornell ya Fasihi ya Afrika mwaka 2022, katika Ukumbi wa Mlimani, jijini Dar es salaam Januari 19, 2023.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi tuzo pamoja na hundi ya Dola 5,000, mshindi wa kwanza wa Ushairi, Salum Makamba, kwenye hafla ya utoaji Tuzo ya Kiswahili ya Safal – Cornell ya Fasihi ya Afrika mwaka 2022, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani, jijini Dar es salaam Januari 19, 2023. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkuu – ALAF Tanzania Ashish Mistry, Mkurugenzi Mkuu SAFAL Group Anders Lindgren, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammed Mchengerwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makala.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...