Wizara ya Afya na Vodacom Tanzania wamekabidhi vyumba vipya 6 baridi ambavyo vitatumika kuhifadhia chanjo. Vifaa hivyo ambavyo vina thamani ya zaidi ya TZS 600 Milioni vilivyotolewa na Vodacom Tanzania Foundation na Vodacom Group, vitahakikisha chanjo zinahifadhiwa kwa usalama hivyo kuimarisha mpango wa Taifa wa chanjo nchini.
Msaada huo uliotolewa na Vodacom
Foundation na Vodacom Group umekuja katika wakati ambao bara la Afrika
linapitia changamoto za uhifadhi wa chanjo kwenye nchi mbalimbali.
Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya duniani (WHO), kanda ya Afrika
kwenye nchi 34 za Afrika umebaini kuwa, katika asilimia 31 ya nchi hizo,
zaidi ya asilimia 50 ya wilaya zake zina changamoto za usambazaji wa
chanjo kutokana na ukosefu wa vifaa vya kuhifadhia madawa hayo.
Usimamizi
wa mnyororo mzima wa vifaa baridi ni sehemu muhimu ya kuhakikisha
usambazaji salama na mzuri wa chanjo. Chanjo zinahitaji majokofu imara
ambayo yanakidhi mahitaji fulani ya joto, kutoka mahali pa utengenezaji
hadi hatua ya mwisho ya usambazaji. Ikiwa mnyororo huu utavunjika wakati
wowote inaweza kuathiri ufanisi mzima wa chanjo na kuzifanya zisiwe na
uwezo za kuzuia maradhi.
"Kama serikali, tunashukuru kuendelea
kuungwa mkono na sekta binafsi katika kufikia malengo ya sekta ya afya
Tanzania na Vodacom wamekuwa wadau wakubwa wa maendeleo ya jamii.
Ninaamini mchango huu kutoka Vodacom Tanzania Foundation utasaidia sana
katika kulinda chanjo dhidi ya athari zinazoweza kuepukika." Nawasihi
watumishi wa sekta ya afya tu kuvilinda vifaa hivyo lakini pia kutumia
nafasi na ushawishi wetu kuhamasisha jamii kujitokeza kupata chanjo,”
alisema Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Vodacom Tanzania Foundation, Harriett
Lwakatare, alisisitiza dhamira ya kampuni hiyo ya kuunga mkono juhudi za
serikali kufikia malengo endelevu ya SDG kwa kubadilisha maisha ya
Watanzania kupitia sekta ya afya.
Juhudi
hizi zinatekelezwa kwa ushirikiano na serikali, mashirika yasiyo ya
kiserikali na washirika wengine wa maendeleo. Juhudi hizi ni pamoja na
kuanzishwa kitaifa kwa mfumo wa usafiri wa dharura ya ‘m-mama’ –
programu ya kiafya ya Vodacom kuhamasisha afya ya uzazi salama kupitia
mradi wa ‘Fistula Inatibika’ na msaada wa kujifungua kabla ya muda
nakadhalika.
“Tunafuraha kwa mara nyingine tena kufanya kazi kwa
ukaribu na Wizara ya Afya katika kuunga mkono mpango wa Taifa wa chanjo.
Mitambo hii ya baridi kali iliyofungwa hapa Dar es Salaam na Zanzibar
itaisaidia serikali katika uhifadhi na usambazaji wa chanjo za kuokoa
maisha, zikiwemo zile zinazotumika kama chanjo kwa watoto,” alisema
Lwakatare.
Hilda Bujiku, Mkurugenzi wa Fedha kutoka Vodacom
kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania Philip Besiimire
alieleza dhamira ya kampuni hiyo katika kuharakisha mafanikio ya SDGs
kwa kuimarisha ushirikiano katika nyanja za afya, elimu, kilimo na
ushirikishwaji wa kifedha. Aidha alihimiza mashirika mengine kuongeza
kasi ya ushirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi kwa manufaa ya
nchi nzima.
Waziri
wa Afya, Mh. Ummy Mwalimu (katikati) akikata utepe kupokea majokofu
sita ya mnyororo wa baridi yenye thamani ya shilingi milioni 600
yaliyosaidiwa na Vodacom Tanzania Foundation na Vodacom Group ambayo
yatatumika kuhifadhia chanjo hivyo kuimarisha mpango wa Taifa wa chanjo
nchini. Pamoja naye kulia ni Mwenyekiti wa Vodacom Tanzania Foundation,
Harriett Lwakatare na kushoto ni Mkurugenzi wa Fedha kutoka Vodacom
Tanzania, Hilda Bujiku.
Waziri
wa Afya, Mh. Ummy Mwalimu (katikati) akizungumza na waandishi wa Habari
(hawapo pichani) wakati wa kupokea majokofu sita ya mnyororo wa baridi
yenye thamani ya shilingi milioni 600 kutoka kwa Vodacom Tanzania
Foundation na Vodacom Group ambayo yatatumika kuhifadhia chanjo hivyo
kuimarisha mpango wa Taifa wa chanjo nchini. Pamoja naye kushoto ni
Mwenyekiti wa Vodacom Tanzania Foundation, Harriett Lwakatare na kulia
ni Mkurugenzi wa Fedha kutoka Vodacom Tanzania, Hilda Bujiku.
Waziri
wa Afya, Mh. Ummy Mwalimu (katikati) akizindua majokofu sita ya
mnyororo wa baridi yenye thamani ya shilingi milioni 600 yaliyosaidiwa
na Vodacom Tanzania Foundation na Vodacom Group ambayo yatatumika
kuhifadhia chanjo hivyo kuimarisha mpango wa Taifa wa chanjo nchini.
Pamoja naye kulia ni Mwenyekiti wa Vodacom Tanzania Foundation, Harriett
Lwakatare na kushoto ni Mkurugenzi wa Fedha kutoka Vodacom Tanzania,
Hilda Bujiku.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...