-Jamii yatakiwa kubeba jukumu la ulinzi wa watoto dhidi ya vitendo vya ukatili

WAZAZI, Walezi na Jamiii kwa ujumla wametakiwa kusimamia ulinzi na usalama wa watoto ili kujenga kizazi bora na salama chenye maadili na tija kwa jamiii.

Hayo yameeelezwa na Diwani wa Kata ya Makumbusho Mohamed Ally wakati wa maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika yaliyoratibiwa na Taasisi ya Wanawake katika Jitihada za Maendeleo (WAJIKI,) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM,) Kata ya Makumbusho na kufanyika katika mtaa wa Sindano.

Amesema katika jitihada hizo WAJIKI wamekuwa mstari wa mbele katika kupambana na vitendo hivyo katika Kata ya Makumbusho kupitia kampeni mbalimbali za ulinzi kwa mtoto na Serikali itaendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha watoto wanakuwa salama.

Amewataka wananchi wa Kata hiyo kufika katika Ofisi za Kata na kupata majibu ya maswali yao pamoja na kupeleka changamoto zao ili ziweze kutambulika na hiyo ni pamoja na kushirikiana na WAJIKI kwa kupeleka changamoto zinazowakabili na kutoa ushirikiano pindi wanapohitajika.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya WAJIKI Janeth Mawinza amesema, maadhimisho hayo yamelenga kuwaleta pamoja wazazi na kutafakari mustakabali wa watoto kwa lengo la kuwajenga kuwa viongozi bora, watendaji na wazazi bora hapo baadaye.

Amewahimiza wazazi na walezi kutenga muda kwa watoto na kuzungumza nao mara kwa mara na kufahamu mienendo yao, marafiki na taaluma kwa ujumla na kudadisi changamoto zinazowakabili wawapo shuleni na nje ya shule.

Aidha amesema WAJIKI inatekeleza kampeni ya 'Safari Salama Bila Rushwa ya Ngono kwa Wasichana na Wanafunzi Inawezekana, Ulinzi wao ni Jukumu Letu,' kampeni ya ulinzi kwa watoto wakike na wanafunzi dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na rushwa ya ngono na kuhimiza ushirikiano baina ya Serikali na wazazi kuanzia ngazi ya Kata kwa kufanyia kazi malalamiko yanayopelekwa hususani ya ukatili wa kijinsia na sio kuyamaliza kifamilia.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya WAJIKI Kalunde Mongomongo amesema, maadhimisho hayo yamewakutanisha wazazi, walezi na wadau na kukumbushana wajibu katika ulinzi na usalama kwa watoto dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

Amesema, kutokana na changamoto ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia WAJIKI imeendelea kupambana dhidi ya vitendo hivyo kwa kuwafikia wadau, waathirika wa vitendo hivyo na kutafuta suluhu ili kujenga jamii bora zaidi.

"Tunaipongeza Serikali kwa kuchukua hatua na mikakati ya kutokomeza ukatili kwa watoto na wanawake kupitia sera na sheria zinazolinda haki za watoto dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji." Amesema.

Pia, ameeleza kuwa mafanikio ya Taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kuunganisha familia zilizofarakana, kufuatilia kesi za matukio ya unyanyasaji wa kijinsia na kufikisha katika maeneo husika, kugundua dalili za unyanyasaji, kuwahifadhi waathirika, kuwafikia wadau katika Wilaya za Ilala na Temeke, kuwafikia wadau wengi zaidi wakiwemo madereva na makondakta wa daladala, bajaji na pikipiki ambao ni wadau wakubwa wa kampeni ya Safari Salama Bila Rushwa ya Ngono kwa Wasichana na Wanafunzi Inawezekana, Ulinzi wao ni Jukumu Letu.

Ameeleza changamoto zinazowakabili ni pamoja na ufinyu wa ufadhili katika utekelezaji wa majukumu, kukosekana kwa eneo la kuwahifadhi wahanga, kukosekana kwa ustadi wa malezi kwa wazazi, kukua kwa teknolojia pamoja na jamii kumaliza kesi za unyanyasaji wa kijinsia kifamilia na kuwaacha wahanga na makovu yasiyopona huku watuhumiwa wakiachwa huru na kuendelea kutenda makosa.

Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu ya 'Zingatia Usalama wa Mtoto katika Ulimwengu wa Kidigitali.'

Taasisi WAJIKI chini ya ufadhili wa Mfuko wa kusaidia wanawake Tanzania (Women Fund Tanzania Trust) wamekuwa mstari wa mbele katika kupambana na vitendo vya ukatili na kijinsia na unyanyasaji wa ngono kwa kushirikiana na wadau.



Diwani wa Kata ya Makumbusho Mohamed Ally akizungumza wakati wa maadhimisho hayo na kuwataka wananchi kutumia Ofisi za Kata na WAJIKI katika kuhakikisha jitihada za kukomesha vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia zinafanikiwa kwa kiasi kikubwa. Leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Jitihada za Maendeleo katika Maendeleo (WAJIKI,) Janeth Mawinza akizungumza wakati wa maadhimisho hayo na kueleza kuwa maadhimisho hayo yamelenga kuwaleta pamoja wazazi, walezi na jamii na kujadili mustakabali Bora kwa watoto. Leo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya WAJIKI Kalunde Mongomongo akizungumza wakati wa maadhimisho hayo na kuitaka jamii kuungana katika jitihada hizo, Leo jijini Dar es Salaam.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...