Na Muhidin Amri, Tunduru
WAKULIMA wa ufuta katika vijiji vya Moland na Lukumbule wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wameingiza zaidi ya Sh.bilioni 6.4 baada ya kuuza kilo 1,626,991.70 katika minada mwili iliyofanyika kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika wilayani Tunduru(Tamcu Ltd)Iman Kalembo alisema,katika mnada wa kwanza uliofanyika kijiji cha Lukumbule wakulima waliuza kilo 857,977.70 zenye thamani ya Sh.bilioni 3,279,190.40. kwa bei ya Sh.3,822.
Alisema katika mnada wa pili uliofanyika katika kijiji cha Molandi kata ya Marumba, wakulima wamefanikiwa kuingiza sokoni kilo 769,014.00 zenye thamani ya Sh.bilioni 3,279,190,770.40 ambapo bei ilikuwa Sh.3,895.
Kalembo alieleza kuwa,katika msimu wa kilimo 2022/2023 lengo ilikuwa kuzalisha tani 350,000 sawa na kilo 3,500,000, lakini kutokana na mwitikio mkubwa wa wakulima katika uzalishaji wanaweza kuvuka malengo waliyojiwekea.
Amewaomba wanunuzi kuongeza bei ili kuwahamasisha wakulima waendelee na uzalishaji wa zao hilo ambalo linaonekana kuwa mkombozi mkubwa kiuchumi kwa wananchi wa wilaya ya Tunduru.
“bei zinapokuwa nzuri wakulima watahamasika kuzalisha kwa wingi zao la ufuta ambalo kwa sasa linaonekana kuwa mkombozi mkubwa kiuchumi kwa wananchi katika wilaya yetu”alisema Kalembo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tamcu Mussa Manjaule,amewataka wakulima wa kijiji cha Molandi kutumia muda wao katika shughuli za kilimo na kuuza mazao yao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ili waweze kupata bei nzuri na hivyo kujikwamua na umaskini.
Alisema,lengo la kujiunga katika vyama vya ushirika ni kutengeneza umoja utakaotetea maslahi ya wakulima na kuuza mazao kwa bei nzuri inayolingana na ghalama za uzalishaji badala ya kuuza kwa bei ya hasara au kupangiwa bei na wanunuzi.
Pia alisema,kupitia vyama vya ushirika wakulima watapata nafasi ya kujifunza namna mbalimbali ya kusimamia mazao yao ili yapate kuwa na thamani sokoni,matumizi sahihi ya fedha na kuirahisishia serikali kupata takwimu za uzalishaji na idadi ya wakulima wake wanaohitaji kupatiwa pembejeo.
Alisema,kijiji cha Molandi ni kati ya maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa ufuta na mazao mengine ya biashara ikiwemo korosho na mbaazi,kwa hiyo kama wataongeza juhudi kwa kupanua mashamba yao na kufanya kilimo chenye tija suala la umaskini katika kijiji hicho litakwisha.
Naye Afisa mazao wa wilaya ya Tunduru Gallus Makwisa,amewapongeza wakulima kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalam wa kilimo ambayo yamesaidia sana kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara wilayani humo.
Alisema,maelekezo hayo yamekuwa chachu ya mafanikio makubwa katika sekta ya kilimo na kuwataka wakulima wa ufuta kuachana na kilimo cha mazoea na kufanya kilimo biashara ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Aidha,amewataka kukumbuka kujiwekea akiba ya chakula kwa ajili ya mahitaji ya familia zao ili kuepuka kununua chakula kwa bei kubwa siku za usoni na kumshukuru Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro kwa kusimamia vizuri shughuli za kilimo na ushirika.
Baadhi ya wakulima,wameishukuru serikali kuendelea kusimamia soko la ufuta kwa mfumo wa stakabadhi ghalani,hata hivyo wameomba malipo yao yafanyike haraka ili fedha watakazolipwa zitumike kufanya maandalizi ya msimu mpya wa kilimo.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Ali Ngonji alisema,licha ya serikali kusisitiza suala la kuuza mazao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani,hata hivyo changamoto kubwa ni kucheleweshewa malipo hali inayochangia kukosa imani na mfumo huo.
Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika wilayani Tunduru Tamcu Ltd Mussa Manjaule akitoa taarifa ya bei ya ufuta katika mnada wa pili wa zao hilo uliofanyika katika kijiji cha Molandi wilayani humo.
Meneja Shughuli wa Chama kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru Tamcu Ltd Mercelino Mrope akitoa taarifa ya mnada wa pili wa zao la ufuta uliofanyika katika kijiji cha Molandi kata ya Marumba ambalo jumla ya kilo 769,014 zenye thamani ya Sh.3,279,190,770.00 zimeuzwa.
Baadhi ya wakulima wa kijiji cha Molandi kata ya Marumba wilayani Tunduru wakifuatilia uendeshaji wa mnada wa ufuta.Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika wilayani Tunduru Tamcu Ltd Mussa Manjaule akizungumza na wakulima wa ufuta kutoka kijiji cha Molandi kata ya Marumba baada ya kukamilika kwa zoezi la mnada wa ufuta. Sehemu ya shehena ya Ufuta uliohifadhiwa katika ghala la Chama Kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...