
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini juu ya mchakato wa uwekezaji kati ya Mamlaka ya Bandari (TPA) na Kampuni ya DP World.
Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai, juu ya uwekezaji bandari nchini, Hamza Johar, akifafanua mchakato wa uwekezaji kati ya Mamlaka ya Bandari (TPA) na Kampuni ya DP World kwa wahariri wa Vyombo vya habari nchini leo Julai 14,2023.
SERIKALI imejibu hoja tatu zilizokuwa zinaibuliwa na wananchi kuhusu mchakato wa uwekezaji kati ya Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) na Kampuni ya DP World.
Imesema kuwa DP World haijapewa zabuni bila kushindanishwa na kampuni nyingine kama inavyodaiwa, bali imepewa uwekezaji huo baada ya kushinda vigezo vya ubora kampuni nyingine kutoka mataifa mbalimbali yaliyojitokeza kuomba nafasi hiyo.
Akizungumza Leo Julai 14,2023 na wahariri wa vyombo vya Habari nchini, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema vigezo alivyoshinda DP World ni pamoja na uzoefu katika utoaji mizigo itakayopitia Bandari ya Dar es Salaam, kisha kuisafirishaji hadi kwa watumiaji.
Amesema wawekezaji wengine walioomba zabuni hiyo ni kampuni kutoka Ufaransa, na UAE lakini hayakukidhi sifa za mwekezaji mahiri atakayehudumia Bandari ya Dar es Salaam kwani hayana uwezo wa uchangiaji mnyororo mzima wa usafirishaji mizigo.
Profesa Mbarawa amesema mkataba huo ni miongoni mwa mikataba 30 iliyosainiwa kati ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai, wakati wa maonyesho ya kimataifa ya Biashara yaliyofanyika Dubai, (Dubai Expo).
Amesema makubaliano hayo hayana masharti ya kuifunga serikali kuhusu ushirikiano katika utekelezaji wa miradi itakayojadiliwa na kukubaliwa na pande mbili.
Waziri Mbarawa ametaja maeneo ambayo DP World hayatakabidhiwa ni gati namba nane hadi 11 katika Bandari ya Dar es Salaam, gati la kupokea mafuta la Kurasini, Bandari ya Tanga, Bagamoyo na Mtwara.
Profesa Mbarawa amesema katika mikataba ya utekelezaji itakayoingiwa baadae, itaweka muda wa utekelezaji, muda wa marejeo baina ya mkataba wa miradi husika. Viashiria muhimu wakati wa utekelezaji wa mikataba.
"Uandaaji wa mikataba utafanywa chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kwa kulinda maslahi ya nchi, mikataba italinda ajira za wazawa. Mifumo ya TEHAMA ya DP itasomana na ya Serikali," amesisitiza.
Akielezea makubaliano hayo, amefafanua kuwa awamu ya kwanza ya makubaliano haya ni kusimamia, kuendesha, kuendeleza gati namba noja hadi saba ya Bandari ya Dar es Salaam, kuboresha magati ya mizigo na abiria kwa lengo la kuvutia shughuli za utalii na kuongeza ufanisi wa bandari kavu.
Awamu ya pili ya ushirikiano ni katika kuongeza thamani ya bidhaa, maeneo ya viwanda, miundombinu itakayowezesha kuongeza ufanisi katika usafirishaji bidhaa nje ya nchi.
Pia, kuweka vyombo vya usafirishaji shehena za mizigo ya maziwa makuu ili kuunganisha bandari zake na nchi jirani.
Waziri huyo ametaja manufaa ya uwekezaji huo, ikiwemo kupunguza muda wa meli kukaa nangani kutoka siku tano mpaka saa 24, utaongeza idadi ya meli zitakazokuja kutoka 1,569 zilizohudimwia 2022, Hadi kufikia 2,950 ifikapo 2032.
Muda wa kushusha makasha (makontena), utapungua kutoka siku Tano Hadi mbili, ushushaji mizigo bandarini utapungua kutoka saa 12 Hadi saa Moja. Gharama za kushusha mizigo zitapungua kutoka Dola za Marekani 12,000 mpaka 6,000 kwa kasha moja kwa mizigo inayokwenda Malawi na Demokrasia ya Congo (DRC).
"Uwekezaji utaongeza shehena zinszohudumiwa kutoka tani 21.8 Hadi 47.57 ifikapo 2032. Mapato ya Serikali yataongezeka kutoka Sh. 7.79 trilioni Hadi 26.7 trilioni ifikapo 2030 na ajira za Watanzania zitaongezeka hadi kufikia zaidi ya 71,000," amesema Mbarawa
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...