Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
BODI ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imeishukuru Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwatengea fedha za kutosha ili kutoa elimu kwa umma kuhusu Bodi hiyo.
Akizungumza na Michuzi Blog jijini Dar es Salaam kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba, Afisa Mipango wa Bodi hiyo, Baraka Ndabila amesema Serikali ya Tanzania imewasaidia pia kutanua mfumo wa Stakabadhi za Ghala.
“Tunaiomba Serikali yetu sikivu kuendelea kucheza nafasi yake hiyo hiyo ya kutuwezesha sisi Bodi ya Stakabadhi, kwa maana Mfumo wa Stakabadhi kwa sasa umetanuka sana na wadau wengi wanaonyesha kuhitaji Mfumo huu,” amesema Ndabila.
“Mfumo wa Stakabadhi, ni nyenzo muhimu ya Kiuchumi katika kuwalinda Wazalishaji na Wakulima kwenye bei zinazobadilika kila wakati, kupitia Mfumo huu wa Stakabadhi unawawezesha Wakulima na Wazalishaji mbalimbali kupata bei halisi ya soko kwa wakati husika,” ameeleza Ndabila.
Ndabila amesema Bodi hiyo ina lengo la kuwafanya wadau mbalimbali wa Kilimo na Wazalishaji wengine wahitaji, waone manufaa na umuhimu wa uwepo wao katika jamii sanjari na kutengeza thamani ya bidhaa zao na kuinua Uchumi kupitia biashara.
Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ni mfumo wa masoko unaowezesha mazao au bidhaa kuhifadhiwa ndani ya Ghala zenye Leseni, Mmiliki wa bidhaa anapewa risiti au Stakabadhi za Ghala zinazothibitisha kuwa bidhaa zilizohifadhiwa katika Ghala husika ni za umiliki mahsusi, thamani yake, aina, idadi na ubora (daraja) ni kama zilivyoandikwa kwenye Stakabadhi.
Mfumo wa Stakabadhi za Ghala umeanza kutekelezwa kwenye zao la Kahawa katika mikoa ya Kilimanjaro na Mbeya kuanzia mwaka 2000 kwa majaribio, mwaka 2007-2008 mfumo huo ulianza kutekelezwa rasmi kwenye zao la Korosho mkoani Mtwara, na baadae Lindi. Mfumo huo umesambaa sehemu mbalimbali nchini na kunufaisha wadau wengi hususani Wakulima.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...