Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
TAASISI ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) imeingia makubaliano ya ushirikiano na Afya Checkers ya jijini Dar es salam kwa ajili ya kutoa huduma za afya kupitia kampeni ya ‘Afya Bora, Maisha Bora’ inayoendeshwa na taasisi hiyo kupitia matembezi ya ‘Mariam Mwinyi Walkathon’.
Matembezi hayo ambayo ni mwendelezo wa kampeni ya mama Mariam aliyokua akiifanya kupitia matembezi ya kila mwisho wa mwezi, yanatarajiwa kufanyika Septemba 30, mwaka huu kwa kutanguliwa na kambi ya matibabu itakayofanyika Septemba 28 na 29.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano hayo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa ZMBF, Fatma Fungo, alieleza hatua hiyo inalenga kuyaimarisha matembezi hayo na kutoa fursa kwa wananchi kupata huduma za afya.
Aidha Fungo alisema katika awamu ya kwanza ya kampeni hiyo, matembezi hayo yalifanyika katika wilaya zote za Zanzibar kwa kushirikisha wadau mbali mbali kwa lengo la kuimarisha afya zao.
“Mara ya mwisho matembezi hayo yalifanyika kisiwani Pemba ambapo watu zaidi ya 3,000 walijitokeza kumuunga mkono mama Mariam Mwinyi (Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapiduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi) katika matembezi na mazoezi ya viungo ili kujenga miili yao”, alieleza Fungo.
Akizungumzia marathoni hiyo, alieleza itafanyika kila baada ya miezi mitatu na kwa lengo la kuyaimarisha yatajumuisha utoaji wa huduma za uchunguzi, upimaji na matibabu wa maradhi mbali mbali zitakazotolewa na wataalamu wa afya kutoka ndani na nje ya Zanzibar.
“Ili kufikia madhumuni ya kampeni hii, tumeamua kushirikiana na wadau mbali mbali wakiwemo Afya Cjheckers ili kuendelea kujenga misingi ya kuimarisha afya za wananchi wenzetu ikiwa ni miongoni mwa malengo ya taasisi yetu”, alieleza Fungo.
Aidha aliishukuru ‘Afya Checkers’ kwa uamuzi wa kushirikiana na taasisi yake jambo alilodai litaongeza kasi ya kampeni hiyo iliyoasisiwa na mama Mariam ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi na Msarifu wa ZMBF.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ‘Afya Checkers’, Dk. Isaac Maro, alieleza kuwa watatumi uzoefu walionao kufanikisha kampeni hiyo ili kutoa fursa kwa wananchi kupata huduma za afya na matibabu kwa urahisi.
Alisema taasisi hiyo toka mwaka 2008/2009 imekua ikijihusisha na masuala ya utoaji wa elimu ya afya na huduma za matibabu kupitia vyombo vya habari na kambi za matibabu kwa kushirikiana na wadau kutoka serikalini na sekta binafsi.
“Muda wote huo tumekua tukitoa hudua za afya na kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu masuala ya afya kupitia kambi maalum zinazojukmuisha madaktari na wataalamu wa afya kutoka hospitali mbali mbali nchini”, alieleza Dk. Maro.
Alitaja miongoni mwa huduma zinazotolewa na taasisi hiyo ni pamoja na uchunguzi wa maradi ya kuambukiaza na yasiyo ya kuambukiza uakiwemo ya UVIKO 19 na huduma za utengamano kwa watoto wenye ulemavu kupitia skuli.
“Pia kupitia kampeni mbali mbali tunafanya tafiti ambazo huwasaidia wadau wakiwemo watunga sera kufanya maamuzi juu ya aina ya huduma za kupeleka kwa jamii”, alieleza.
Aidha alipongeza ZMBF kwa juhudi inazochukua kuimarisha jamii kupitia kampeni na programu mbali mbali hususani za afya jambo linaloongeza thamani ya taasisi hiyo mbele ya jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya ZMBF, Nassir Ahmed Haji, ambaye ni Mjumbe wa Bodi, alipongeza hatua hiyo na kuahidi kwamba bodi itatoa kila aina ya ushirikiano kufanikisha utekelezaji wake.
Hivyo aliwataka wadau wengine kuendelea kuunga mkono kampeni hiyo kwa kuwa ina faida kwa jamii ikiwa ni miongoni mwa malengo ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
MJUMBE wa Bodi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Nasir Ahmed Haji (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Fatma Fungo (kushoto) na Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Afya Checkers, Dk. Ramona Malikusema (kulia) pamoja na watendaji wengine wa taasisi hizo baada ya hafla ya utiaji saini wa hati za makubaliano ya ushirikiano ya utekelezaji wa kampeni ya ‘Afya Bora Maisha Bora’ iliyofanyika katika ofisi za ZMBF, Migombani Zanzibar.
OFISA Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Fatma Fungo (kulia) na Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Afya Checkers, Dk. Ramona Malikusema, wakisaini makubaliano ya ushirikiano ya utekelezaji wa kampeni ya ‘Afya Bora Maisha’ inayotekelezwa na ZBMF wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo iliyofanyika katika ofisi za ZMBF, Migombani Zanzibar.
OFISA Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Fatma Fungo (kulia) na Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Afya Checkers, Dk. Ramona Malikusema, wakionesha hati za makubaliano ya ushirikiano ya utekelezaji wa kampeni ya ‘Afya Bora Maisha Bora’ inayotekelezwa na ZBMF wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo iliyofanyika katika ofisi za ZMBF, Migombani Zanzibar.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...