Na Mwandishi wetu, Simanjiro
HALMASHAURI ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, imejipanga kutatua kero na changamoto mbalimbali zilizopo kwa wananchi wa kata zake 18 kupitia mpango wa bango kitita.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Gracian Makota ameyasema kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika mji mdogo wa Orkesumet.

Makota amesema kwa kutumia bango kitita wataorodhesha mawasilisho, malalamiko, kero na changamoto mbalimbali za madiwani na kuzifanyia kazi ili kuhakikisha wananchi wanatekelezewa wajibu wao.

"Tumeandaa bango kitita ambayo italeta tija kwenye kata zetu kwani mimi na wataalamu wangu tutakaa pamoja kuhakikisha mahali penye kero na changamoto tunashughulikia," amesema Makota.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga amempongeza mkurugenzi Makota kwa kasi kubwa ya maendeleo aliyokuja nayo Simanjiro hivyo madiwani wamuunge mkono.

Diwani wa kata ya Ngorika amewaasa viongozi wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanajipanga kuacha alama kwa jamii kwa kujenga vituo vingi vya afya wilaya ya Simanjiro.

Diwani wa kata ya Mirerani Salome Mnyawi amesema wataalamu wa ardhi wanapaswa kupima na kuhakiki eneo walilopatiwa na shirika la Light In Africa ili lisivamiwe na wajenge kituo cha afya.

Diwani wa kata ya Loiborsiret, Ezekiel Lesenga (Mardadi) ameitaka wakala wa barabara za mjini na vijijini (Tarura) kuweka alama za barabarani kwani hivi karibuni ng'ombe 25 ziligongwa na basi.

Diwani wa kata ya Loiborsoit, Siria Kiduya, amesema wana changamoto ya daraja la kuunganisha kata hiyo na wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Diwani wa kata ya Orkesumet Sendeu Laizer amesema zaidi ya kuwa na miradi ya maendeleo hivi sasa hawana changamoto zinazowakabili.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...