Na Mwandishi wetu, Simanjiro

SHULE mbili za msingi Naisinyai na Oloshonyokie za Kijiji cha Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wanafunzi wake wamenufaika na msaada wa vyakula na mafuta vilivyotolewa na kampuni ya Franone Mining and Gems LTD.

Msaada huo wa magunia 120 ya mahindi, magunia 20 ya maharage na ndoo 20 za lita 400 za mafuta ya kupikia umetolewa na kampuni hiyo ya uchimbaji madini ya Franone Mining and Gems LTD inayochimba madini ya Tanzanite kwemye kitalu D na wamiliki wa kitalu C.

Mwenyekiti wa kijiji cha Naisinyai, Merika Makeseni amesema msaada huo umekuja kwa wakati muafaka hivyo wanaishukuru kampuni ya Franone Mining and Gems LTD.

Merika amesema kwa moyo wa dhati na kwa niaba ya jamii nzima ya wana Naisinyai, anawashukuru wakurugenzi na uongozi wa kampuni ya Franone Mining and Gems LTD kwa msaada mkubwa waliotoa kwa shule zao mbili za msingi Naisinyai na Oloshonyokie.

"Kimsingi maeneo yetu kama yalivyo maeneo mengi ya nchi yetu kwa miaka mitatu yamekumbana na changamoto ya ukosefu wa chakula hali iloyotokana na mvua kuwa chache kutokana na nchi kukabiliana na mabadiliko makubwa ya tabia nchi," amesema Merika.

Amesema hali hiyo pia imesababisha mifugo mingi ambayo ni tegemeo kubwa kwa jamii ya wafugaji kufa na michache iliyobaki kudhoofu kiasi cha kutouzika kirahisi na kwa bei rafiki.

Amesema kutokana na hali hiyo wakaamua kuwashirikisha wadau wa maendeleo kwa mwaka huu walau waweze kusadia chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule za msingi ambao kwa kawaida huchangiwa na wazazi.

"Niwashukuru viongozi wenzangu waliotupa ushirikiano katika hili ambao ni mheshimiwa mkuu wa wilaya Suleiman Serera, mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri Gracian Makota, Ofisa tarafa Moipo Dhulfa Laizer na mheshimiwa Diwani wa kata Taiko Laizer kwa namna walivyojitoa kuhakikisha tunafanikisha hili," amesema.

Amesema ni ahadi yake na kamati za shule kuwa chakula hicho watakisimamia kukihifadhi na kuhakikisha kuwa kitatumika kwa lengo lililokusudiwa.

"Ni maombi yetu kwa Mungu wetu kuwabariki kampuni ya Franone Mining and Gems LTD na kuwajazilizia wale waliokitoa ili wasijutie wao kwa kutoa sadaka hii kubwa kwa watoto wetu," amesema Merika.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Naisinyai, Agnes Chang'endo ameishukuru kampuni ya Franone Mining and Gems LTD kwa msaada huo wa chakula cha wanafunzi hao.

Makamu Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Tauta Siria amesema watahakikisha chakula hicho kinatumika ipasavyo kwa lengo husika lililokusudiwa.

Mmoja kati ya wanafunzi wa shule ya msingi Oloshonyokie, James Loishiye amesema msaada huo wa chakula utakuwa kichocheo kwa wao kuhudhuria masomo shuleni.

"Mwanafunzi akija shule atafundishwa na mwalimu, atasoma na kuandika, atakula chakula na kucheza, hivyo lazima atahudhuria masomo shuleni," amesema Loishiye.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...