Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
UPENDE wa Jamuhuri katika kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka saba ikiwemo kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh Milioni 954.5.

inayowakabili mafundi wa mashine za kielektroniki za EFD na mwanamke mmoja wamefanyia mabadiliko hati ya mashtaka kwa kumuongeza mfanyabiashara Frank Kalage

Mshtakiwa Kalage amesomewa mashtaka manne leo Januari 23, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Is-hqa Kuppa na wakili wa serikali Mwandamizi Job Mrema akisaidiana na wakili wa serikali Emmanuel Medalakini pamoja na Auni Chilamula.

Mshtakiwa Kalage ataunganishwa na washtakiwa wenzake Februari 7,2024 ambao ni Awadhi Mhavile, Ally Msesya maarufu kama Ally Yanga (37) mafundi wa mashine za EFD na Salma Ndauka (38) Msimamizi wa Gereji anayeishi Sinza ambapo kwa leo hawakuweza kufika mahakamani kufuatia changamoto za usafiri kutoka gerezani.

Mashtaka dhidi ya Kalage yamesomwa na Wakili Mrema ambapo ameunganishwa kwenye mashtaka ya kutumia isivyohalali mashine za EFD zilizozuiwa na kumpotosha Kamishina, kumdanganya Kamishna wa TRA kwa kutoa risiti zisizo sahihi na kuwanufaisha walipa kodi wengine kudai Sh 954,596,372, kuisababisha TRA hasara na utakatishaji fedha.

Wakili Mrema alidai washitakiwa wametenda makosa hayo kati ya Mei na Julai mwaka 2023 ndani ya jiji la Dar es Salaam.

Inadaiwa kuwa kati ya Mei 17 na Julai 2023, katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, washitakiwa wote kwa pamoja walitumia isivyohalali mashine za EFD zilizozuiwa kinyume na sheria kutengeneza risiti zisizo halali zilizopakiwa kwenye mfumo wa TRA na kuwezesha walipa kodi wengine kudai Kodi ya Ongezeko la Thamani ya Sh 954,596,372 na kumpotosha Kamishina wa mamlaka hiyo.

Pia washitakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kutumia isivyo halali mashine za EFD zilizokuwa zimefungiwa na kumdanganya Kamishna wa TRA kwa kutoa risiti zisizosahihi hivyo, kuwanufaisha walipa kodi wengine kudai Sh 954,596,372.

Aidha katika mashitaka ya tatu yanayomkabili Mhavile peke yake inadaiwa, Julai 8 mwaka 2023, mshatakiwa huyo alikutwa na mashine za kielektroniki 22 zinazozaniwa kuwa za wizi au zimepatikana kwa njia isiyo halali.

Wakili alidai kudai kuwa, Julai 19, mwaka jana maeneo ya Sinza A, Wilaya ya Kinondoni, Ndauka alikutwa na mashine 10 za EFD zidhaniwazo kuwa za wizi au kuchukuliwa kwa njia ya isivyohalali.

Mshtakiwa Mhavile anadaiwa pia Julai 8 mwaka 2023 maeneo ya Lumumba mkoani Dar es Salaam, alikutwa na mashine 10 za EFD na kutoa risiti za kielektroniki kinyume na sheria.

Aliendelea kudai kuwa washitakiwa wote kwa pamoja kati ya Mei 13 na Julai mwaka 2023, mkoani Dar es Salaam, washitakiwa Mhavile, Ndauka na Msesya waliisababishia serikali (TRA) hasara ya Sh milioni 954.5.

Katika mashitaka ya utakatishaji fedha, inadaiwa kati ya Mei 13 na Julai mwaka 2023, jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa kutumia mashine hiyo walitoa risiti zisizohalali zilizotumiwa na walipakodi wengine kudai Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya Sh milioni 954.5 kwa TRA wakati wakijua kwamba fedha hizo ni zao la kosa la kuisababishia serikali hasara.

Hata hivyo mshitakiwa huyo hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi hadi kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na hakimu Kuppa ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 7, 2024 .na washitakiwa wataendelea kukaa rumande kwa kuwa mashitaka hayo hayana dhamana kisheria.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...