Na Mwandishi wetu

Benki ya Diamond Tust (DTB) imetoa wito kwa wasichana pamoja na wanawake wanaosoma masomo ya sayansi kutokukata tamaa na kuongeza juhudi  ili kufikia malengo yao.

Jesca Tugara, Kaimu Mkuu Kitengo cha Mawasiliano na Masoko kutoka benki ya DTB ametoa wito huo leo Februari 11, 2024 jijini Dar es Salaam wakati baadhi ya wafanyakazi wa benki hiyo kitengo cha Tehama walipotembelea shule ya sekondari ya wasichana Alpha ili kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana Katika Sayansi.

Amesema lengo la tukio hilo ni kutambua mchango wao katika sekta ya sayansi na kuwapa moyo ili waweze kupata ujasiri wa kusonga mbele bila kuwa na woga wowote.

“Tukiwa tunaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana Katika Sayansi tunataka muishi kwenye ushuhuda wetu tutakaowapatia leo ili muweze kupata moyo kwa kile mnachokifanya na kusonga mbele,” amesema Tugara.

Solana Mpepo, mfanyakazi wa benki ya DTB kitengo cha Tehama ameainisha ujuzi , uwezo na umakini endelevu kama mambo muhimu ya kuzingatia ili kufikia malengo yao.

“Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana Katika Sayansi, inatupa ujasiri kama watendaji katika sekta ya sayansi kuwaeleza kuwa kupitia ujuzi na muendelezo wa kile mnachokifanya hakuna linaloshindikana,” amesema Mpepo.

Aliongeza: “Fani haina ugumu wowote. Ninachotaka kusisitiza ni kwamba sayansi inamuhitaji mwanamke na mwanamke anahitaji sayansi.”

Jenny Nsemo, mwanafunzi wa sekondari ya wasichana ya Alpha mchepuo wa Fizikia, Kemia na Hisabati (PCM) amesema kinadharia sayansi ni ngumu tofauti na uhalisia wke.

 “Watu hudhani Hisabati ni ngumu lakini ni fani rahisi sana na faida zake zipo katika sekta nyingi ulimwenguni,” amesema Nsemo.

Februari 11 kila mwaka ni siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana katika Sayansi. Lengo likiwa ni fursa kwa wote kuchukua msimamo kwa ajili ya wasichana na wanawake katika sekta hii muhimu.

Katika kuadhimisha siku hii iliyopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2015, Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni, UNESCO limesema wasichana wanaendelea kukumbwa na ubaguzi, vikwazo vya kijamii na kitamaduni ambavyo vinawazuia kupata elimu na fedha za kufanya utafiti na kuwazuia kuingia katika kazi zitokanazo na masomo ya sayansi na hivyo kuwakwamisha kufikia uwezo wao kikamilifu.

Mwisho.

Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya Diamond Trust (DTB) kitengo cha Tehama wakiwa pamoja na wanafunzi wa kidato cha tano na sita wa shule ya sekondari ya Alpha iliyoko Kunduchi Dar es Salaam katika hafla fupi iliyoandaliwa na benki hiyo leo jijini humo kuadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana katika sayansi. (Kulia) ni Kaimu Mkuu Kitengo cha Mawasiliano na Masoko benki ya Diamond Trust (DTB) Jesca Tugara. Picha: Mwandishi wetu.


Kaimu Mkuu Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa Benki ya Diamond Trust (DTB), Jesca Tugara (kushoto), akiuliza maswali kuhusu fani ya sayansi kwa mmoja wa wanafunzi wa kidato cha tano na sita wa Shule ya Sekondari ya Alpha ya Kunduchi, wakati wafanyakazi kitengo cha Tehama cha benki hiyo, walipoadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana katika sayansi, shuleni hapo, Dar es Salaam leo


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...