Baadhi ya mafundi wakiendelea na kazi ya kuchimba kisima kirefu cha maji katika soko hilo ikiwa ni mpango wa Halmashauri ya wilaya katika kukabiliana na uhaba wa maji safi na salama.
Gari maalum linalotumika kwa ajili ya utafiti wa maji na uchimbaji wa visima likiendelea na kazi ya kutafuta maji katika eneo la soko kuu la Azimio Tunduru mjini.

Na Mwandishi Wetu, Tunduru
SERIKALI kupitia Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,imetenga zaidi ya Sh.milioni 80 kwa ajili ya kuchimba visima vinne vya maji ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa mji wa Tunduru.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru Chiza Marando alisema,miongoni mwa maeneo hayo ni soko kuu la Azimio,soko la Nanjoka,kituo kikuu cha mabasi na maeneo mingine yanayotumika kupakia na kushushua watu wanaotoka pembezoni mwa mji wa Tunduru.

Marando alisema,wameamua uchimba visima hivyo katika maeneo tofauti na maji hayo yataingizwa kwenye mfumo wa mabomba kabla ya kusambazwa kwenda kwa wananchi watakaohitaji kuunganishiwa huduma ya maji.

Alisema,wameamua kushirikiana na mamlaka ya maji mjini Tunduru(MTUWASA)kuhakikisha wanapunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji katika mji wa Tunduru ambao kwa muda mrefu wananchi kumekuwa na mgao mkubwa wa maji.

“Visima tunavyochimba tunataka vitumike kupunguza changamoto kubwa ya huduma ya maji kwenye maeneo yenye msongamano,lengo letu ni kuona wananchi wa mji wetu wa Tunduru wanapata huduma ya maji kwa masaa 24”alisema Marando.

Aidha alieleza kuwa,maji hayo yatauzwa na kuwa sehemu ya chanzo cha mapato ya Halmashauri na kwa sasa Halmashauri ya wilaya ipo kwenye mazungumzo na mamlaka ya maji ili kuona namna gani wanavyoweza kushirikiana katika uendeshaji wa mradi huo.

Marando,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa magari ya kuchimba visima vya maji kwa kila mkoa hapa nchini na amewaomba wananchi kushirikiana na serikali yao katika ulinzi wa visima na miundombinu ya maji itakakayojengwa katika maeneo mbalimbali.

Msimamizi wa uchimbaji visima kutoka wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kanda ya kusini Thomas Masheyo alisema,utafiti unaonyesha eneo kubwa la mji wa Tunduru kuna maji mengi ambayo yanatosheleza mahitaji ya watu wa mji huo.

Ameshauri wananchi wanaotaka kuchimba visima ni vyema wakazingatia ushauri wa wataalam kwa kuchimba visima virefu badala ya vifupi kwa kuwa maji ya juu yanayopatikana kwenye visima vifupi siyo salama sana kwa matumizi ya binadamu ikilinganisha na maji yanayopatikana kwenye visima virefu.

Mfanyabiashara wa soko la Azimio Andrew John alisema,maji hayo yatamaliza adha kubwa ya maji katika soko hilo ambalo kwa muda mrefu halina maji ya uhakika.

Alisema,wakati mwingine baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo wanalazimika kurudi nyumbani au kwenda kwenye bar kila wanapotaka kupata huduma ya choo.

Said Kadebeje alisema,katika soko hilo kuna vyoo viwili tu ambavyo kutokana na idadi ya watu waliopo kwa sasa havitoshelezi hasa pale wanapotaka kujisaidia kutokana na kukosa huduma ya maji.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...