Naibu wa Waziri wa Habari ,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Methew akizungumza wakati mkutano wa mwaka wa Vyombo vya Utangazaji nchini uliofanyika Jijini Dodoma.
Mkuu  wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza wakati Mkutano wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji Nchini uliofanyika jijini Dodoma.
Mkuu wa Kitengo cha Leseni za Mawasiliano TCRA Mhandisi Andrew Kisaka akitoa maelezo kuhusiana na hali ya vyombo vya utangazaji katika mkutano wa mwaka wa vyombo vya utangazaji uliofanyika jijini Dodoma.
Picha za vyeti pamoja na picha za pamoja za Makundi Mbalimbali katika Mkutano wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji uliofanyika jijini Dodoma

Picha za vyeti pamoja na picha za pamoja za Makundi Mbalimbali katika Mkutano wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji uliofanyika jijini Dodoma

Na Mwandishi Wetu – DODOMA
MKUTANO Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji nchini umefunguliwa rasmi na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew, katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini hapa. Mkutano huo wa siku mbili uliowakutanisha watoa huduma za utangazaji nchini umegusia masuala muhimu kuhusu maendeleo ya utangazaji na mageuzi ya kiteknolojia.

Katika hotuba yake, Mhandisi Kundo Mathew alitangaza kwamba matangazo ya redio yamefikia asilimia 55 ya eneo la kijiografia la Tanzania, isipokuwa maeneo ya mbuga za wanyama na misitu. Aidha, alifafanua kuwa Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ipo katika hatua za mwisho kukamilisha mapitio ya Kanuni za Utangazaji, kuruhusu matumizi ya teknolojia ya utangazaji wa redio kidijitali, maarufu kama 'Digital Sound Broadcasting (DSB)'. Teknolojia hiyo ilielezwa itapunguza changamoto ya ukosefu wa masafa ya redio, hasa katika maeneo ya miji mikubwa nchini hivyo kuongeza wigo mpana zaidi wa ufikishaji wa maudhui ya redio kwa wananchi wengi zaidi yakiwemo maeneo ya mpakani.

DSB ni teknolojia inayotumia miundombinu ya kidijitali kama vile mkongo wa mawasiliano ili kufikisha maudhui kwa mlaji ambae ni Mwananchi badala ya kutegemea masafa ya redio pekee ili kufikisha maudhui kwa msikilizaji. Mhandisi Andrew Kisaka wa TCRA akielezea teknolojia hiyo pembezoni mwa Mkutano huo alieleza kuwa itawawezesha watoa huduma wengi zaidi kutoa matangazo na kuongeza uwezekano wa kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Akizungumzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, Mhandisi Mathew alisisitiza umuhimu wa sekta ya utangazaji kuifanikisha uchaguzi huo unaotarajiwa baadae mwaka huu na kuwataka wadau wa sekta hiyo kuwa kipaumbele katika kufikisha maudhui bora yanayohusu shughuli za uchaguzi na maendeleo kwa wananchi wakati wa uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani.

Katika juhudi za kuboresha sekta ya utangazaji, Mhandisi Kundo alitangaza kwamba Serikali imeagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufanya Upembuzi Yakinifu wa sekta yote ya utangazaji. Hii itahusisha kutumia Mshauri Mwelekezi wa Kimataifa kuchunguza changamoto zinazokabili sekta hiyo, kuzingatia mageuzi ya kiteknolojia, vyanzo vya mapato, gharama za uendeshaji, soko la utangazaji, utandawazi, na maudhui ya utangazaji na athari zake ili kuona uwezekano wa kutatua changamoto za Utangazaji zikiwemo zinazohusu uwezo wa vituo vya Utangazaji kujiendesha kimapato.

Mhandisi Kundo aliwaasa wadau wa sekta ya utangazaji kushiriki kikamilifu katika mchakato huo wa kuboresha sekta na kutoa maoni yao kwa kushirikiana na Mshauri Mwelekezi atakapokuwa akitekeleza majukumu yake chini ya usimamizi wa TCRA.

Mkutano wa Vyombo vya Utangazaji, uliowakutanisha watoa huduma mbalimbali wa utangazaji nchini, ulihitimishwa na azimio la kuunganisha jitihada za pamoja kuhakikisha vyombo vya utangazaji vinazingatia maadili na kuondoa maudhui yanayokiuka viwango vya utangazaji.

“Tunatarajia kuona maendeleo makubwa katika sekta ya utangazaji nchini Tanzania wakati teknolojia mpya na mikakati ya kuboresha vinapojengwa na kutekelezwa,” alieleza Jacob Mwenga Meneja wa kituo cha Utangazaji cha Ice kilichopo Makambako, Njombe.

Mkutano wa Mwaka wa Utangazaji huandaliwa kila mwaka na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, ukiwaleta pamoja wadau wa sekta ya Utangazaji nchini Tanzania ili kujadili changamoto na fursa za sekta hiyo, na kuiwezesha Mamlaka ya Mawasiliano kuweka mikakati ya kuboresha zaidi sekta hiyo.

Mkutano huo watoa huduma za utangazaji nchini walikubaliana kuhakikisha vituo vya utangazaji vinaweka kipaumbele kulinda maadili ya jamii wakati wa kutekeleza shughuli za utangazaji

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...