Na. Beatus Maganja
MKUU wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Emil Ngubiagal amesema Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA ni taasisi iliyoleta mapinduzi makubwa katika Sekta ya Utalii na kuwa chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali na wazawa wa wilaya hiyo kutokana na maboresho ya miundombinu ya utalii katika Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara yanayopelekea watalii wengi kutembelea Hifadhi hiyo.

Komredi Ngubiagal ameyasema hayo Februari 25, 2024 akizungumza na waandishi wa habari wilayani humo ikiwa ni siku moja baada ya meli iliyobeba watalii 146 kutia nanga katika Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara.

"Naipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa awamu ya sita kwa kuona sasa utalii katika wilaya ya Kilwa ni vyema tupeleke taasisi inayoitwa TAWA ili kusudi ikasimamie, ikaendeleze, ikaboreshe hii Sekta nzima ya utalii ya wilaya ya Kilwa" amesema Mhe. Christopher Ngubiagal

"Kwakweli kwasasa hivi unavyoona maendeleo makubwa katika Sekta hii ya utalii Kilwa yameletwa na Taasisi ya TAWA, Leo ukifika Kilwa kisiwani utaona mabadiliko makubwa katika miundombinu" ameongeza Mkuu huyo wa wilaya.

Mhe. Christopher amesema awali kabla ya ujio wa TAWA wakazi wa wilaya yake pamoja na watalii walikuwa wakipata adha ya kufika Kilwa kisiwani kutokana na uduni wa miundombinu lakini baada ya kuingia TAWA walipeleka boti za Kisasa ambazo zinawafanya watalii na wazawa hao kufika hifadhini kwa raha mstarehe.

Aidha amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza soko la utalii aliposhiriki filamu ya Tanzania The Royal Tour ambayo imeleta mabadiliko makubwa ambayo hayajawahi kutokea.

Naye Said Amri Said mkazi wa Kilwa kisiwani amekiri kuwa ujio wa TAWA katika Hifadhi hiyo umechangia kuongeza idadi ya watalii ambapo kupitia wageni hao wakazi wa eneo hilo wananufaika kiuchumi kwa kufanya biashara ndogo ndogo ambazo zinawaingizia kipato.

Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja ametoa wito kwa wakazi wa wilaya ya hiyo kutumia fursa ya ujio wa Meli za watalii kujiongezea kipato kwa kuuza bidhaa pendwa kwa wageni kama vile vitu mbalimbali vya asili na kiutamaduni.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...