Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha.


WAKAZI wa Kitongoji cha Kisabi , Mlandizi,Kibaha Vijijini , Mkoani Pwani wanaotakiwa kupisha eneo hilo na kuhamia Kikongo eneo lenye ekari 1,000 lililotolewa na Serikali wamegomea kuhama wakidai ugumu wa kuanza maisha mapya.

Hayo yalielezwa na wakazi hao akiwemo Esther Shishima, Nuhu Msheka ,Daudi Mwasumbi wakati Mkuu wa wilaya Kibaha Nikkison Simon alipomwakilisha Mkuu wa mkoa wa Pwani Alhaj Abubakar Kunenge kwenye mkutano wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Shishima aliiomba, Serikali kuwaacha waendelee kuishi katika eneo hilo kwani wamechoka kuhamahama na watoto kama wakimbizi.

"Tunaambiwa tuhame kuwa kuna zuio la kimazingira tuache kuendelea kujenga,eti sheria imekataa ,sasa mbona wapo wenzetu eneo la  Halmashauri wanajenga na wanamudu hiyo hali ,basi na sisi tutaweza,watuache tumechoka kuhangaika na watoto" alifafanua Shishima.

Nae Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kisabi ,Yahaya Matata alieleza awali waliovamia eneo hilo walikuwa 41 baadae wakaongezeka na kufikia 91 sasa wameongezeka wapo zaidi ya 300.

Mkuu wa wilaya ya Kibaha , Nikkison aliahidi kuyafikisha maombi hayo sehemu husika kwa lengo la kutoa maamuzi zaidi ingawa alisisi kuwa kutokana na ushauri wa kitaalam kimazingira eneo hilo si rafiki kwa makazi hiyo wananchi wanapaswa kuhama.

Nikkison alieleza Serikali ya mkoa ilitoa ekari 1,000 kwa wakazi wa Kisabi ili lipimwe viwanja na kugawiwa kwa wakazi wanaoishi kwenye eneo Oevu.

Nikkison alifafanua kuwa, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa mazingira- NEMC lilitahadharisha juu ya eneo hilo kutumika kujengwa makazi ya binadamu kwa kuwa ni oevu linaloweza kusababisha madhara yatokanayo na mafuriko kikiwa ni pamoja na uwezekano wa nyumba kutitia.

Kutokana na hali hiyo Ofisi iliamua kutafuta eneo rafiki linalofaa kwa makazi ya binadamu ambalo alieleza linapatikana katika kijiji cha Kikongo na sasa maandalizi ya upimaji unaendelea ili wakazi hao wapewe viwanja.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...