WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Wahandisi la Kimataifa la 14 litakalofanyika jijini Arusha Desemba 4 hadi 6, 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Novemba 25, 2024 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET), Ipyana Moses, amesema kuwa kongamano hilo litahudhuriwa na watu zaidi ya 1000, wengine baadhi watashiriki kwa njia ya mtandao.
"Tunatazamia wahandisi, mafundi, wanafunzi na wadau wengine kutoka mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi watashiriki kongamano hilokatika Ukumbi wa Kimataifa Arusha (AICC)." Amesema
Aidha amewakaribisha Wahandisi na wadau wote wa sekta mbalimbali za uchumi nchini kuhudhuria katika kongamano hilo la kimataifa.
Katika kongamano hilo kutakuwa na mada zilizochaguliwa kutoka kwa wawasilishaji wabobezi katika tasnia hiyo.
"Pamoja na mambo mengine, mada zimejikita katika kutoa elimu ya ubunifu na zinalenga kuhimiza na kuchochea ari ya
kuondoa dhana ya ufanyaji kazi kwa mazoea na kusisitiza kuzingatia ubunifu, nidhamu, umakini, ufanisi, uwezo, juhudi, weledi na uwajibikaji katika kila nyanja, ili kuboresha au kuibua suluhu mpya katika utekelezaji wa kazi mbalimbali za kihandisi.
Hii itafungua njia katika safari ya kufikia maendeleo endelevu na kuifanya Tanzania kuwa mshindani katika ngazi za kikanda na kimataifa, ikidhihirisha kama mshiriki hai katika nyakati hizi za utandawazi. Vinginevyo, Tanzania kama nchi tutabaki kama watazamaji wa utandawazi na kuendelea kutegemea nguvukazi/wataalamu kutoka nje ya nchi." Ameeleza Ipyana
Dhima ya kongamano hilo ni "Elevate and Innovate Engineering Excellence in a Dynamic World" 'Kuza na Fanya Ubunifu: Uhandisi Bora Katika Dunia Inayobadilika.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...