

KATIKA kufanikisha uandishi wa kidigitali, waandishi wa habari wanahimizwa kuwekeza katika kujiajiri badala ya kutegemea ajira za kawaida.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Profesa Eliamani Sedoyeka, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari. Mafunzo hayo yalifanyika katika chuo cha IAA yalilenga kuwawezesha waandishi wa habari kutumia mitandao ya kijamii kwa ufanisi, kufuata maadili ya mitandao ya kijamii, na kujitengenezea ubora katika kazi zao.
Prof. Sedoyeka amesisitiza kuwa uandishi wa kidigitali ni nyenzo muhimu kwa waandishi wa habari wa kisasa, kwani unarahisisha usambazaji wa habari na kuongeza ufikiaji wa wasikilizaji. Aidha, ameongeza kuwa mitandao ya kijamii ina nafasi kubwa katika kuongeza fursa za kujiajiri, hivyo waandishi wanapaswa kuwa na uwezo wa kutumia teknolojia mpya za kidigitali ili kubaki kwenye ushindani wa soko la ajira.
Prof. Sedoyeka pia ameeleza kuwa Chuo cha IAA kinatambua mabadiliko katika teknolojia, na kwa hiyo kimeona umuhimu wa kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari ili waweze kufanya kazi zao kwa kufuata misingi na taratibu sahihi, ingawa mitandao ya kijamii mara nyingi hufuata utaratibu wa habari tofauti.
Amefafanua kuwa chuo hicho kinazidi kukua na kujiimarisha kwa kasi, hasa kutokana na kuanzisha kozi ambazo zinalenga kubadili mtazamo wa wanafunzi kuhusu soko la ajira na kuwawezesha kuwa sehemu ya wazalishaji wa ajira badala ya kutegemea ajira.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...