Farida Mangube, Morogoro

Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Jesper Kamp, ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa ilizopiga katika kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia sekta ya mifugo, hatua inayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa vijana wa Kitanzania.

Balozi Jesper ametoa pongezi hizo Mkoani Morogoro kwa niaba ya mabalozi wenzake kutoka nchi za Nordic ambazo ni Denmark, Norway, Sweden na Finland walipotembea Ushirika wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUGECO).

“Tumeona matokeo chanya katika uwezeshaji wa vijana kupitia sekta ya mifugo. Hii ni hatua muhimu katika kupambana na ukosefu wa ajira na kuleta maendeleo endelevu,” alisema Balozi Jesper.

Aidha, mabalozi hao walieleza dhamira yao ya kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika maeneo ya misitu, tafiti, kilimo na maendeleo ya jamii, huku wakiahidi kusaidia juhudi zinazolenga kuimarisha mazingira na uendelevu wa rasilimali asilia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa SUGECO, Revocatus Kimario, amesema ushirikiano na nchi hizo umekuwa wa manufaa makubwa, akibainisha kuwa zaidi ya vijana 850 wamepelekwa nje ya nchi hizo kwa mafunzo na uzoefu wa kilimo cha kisasa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Kati ya hao, vijana 535 walipelekwa mwaka 2023 pekee.

“Kwa sasa tupo kwenye hatua za mwisho za kuanzisha kituo cha umahiri wa uzalishaji wa mbegu bora za nguruwe hapa Morogoro, kwa kushirikiana na kampuni kutoka Denmark,” alisema Kimario.

Katika ziara hiyo, mabalozi hao walitembelea pia kituo cha kuzalisha mbegu za miti kilichopo chini ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ambapo walishiriki shughuli za upandaji miti kama ishara ya kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa mazingira.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...