Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Rukwa
JAJI Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Dkt. Mustapher Siyani ametoa wito kwa Viongozi wa Umma na Wananchi kwa ujumla kujiepusha kuzungumzia au kutoa misimamo juu ya mashauri yanayoendelea mahakamani.

Akizungumza kwenye Mkutano wa Tume na wadau wa utoaji haki mkoani Katavi jana tarehe 28 Mei, 2025, Jaji Kiongozi amesema kumekuwa na mazoea kwa Vongozi wa Umma na wananchi kutoa matamko juu ya mashauri yanayoendelea mahakamani hali ambayo inawaweka katika wakati mgumu Majaji na Mahakimu wanaosikiliza mashauri kutoa uamuzi huru.

Alisema mara nyingi jamii imekuwa ikiamini matamko yanayotolewa na Viongozi na hivyo kutarajia uamuzi wa shauri husika kuwa kama vile maoni, matamko au misimamo iliyotolewa na Viongozi.

Jaji Kiongozi alisema Tume ya Utumishi wa Mahakama na Mahakama ya Tanzania inatarajia kuona Viongozi wote na wananchi kwa ujumla wakijizuia kutoa matamko, maoni au misimamo kwenye mashauri yanayoendelea mahakamani ili kulinda uhuru wa Mahakama na kujenga imani ya wananchi kwa Mhilimili huo wenye kauli ya mwisho juu ya utoaji haki nchini.

Aidha alisema Tume na Mahakama pia inatarajia kuona kuwa wananchi na viongozi wa Umma wataimarisha ushirikiano na Mahakama katika maboresho ya huduma za zake yanayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumzia nafasi ya Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya, Jaji Kiongozi ametoa wito kwa Kamati hizo kuanza kutazama visababishi vya uhalifu badala ya kujikita katika ukamataji na upelelezi baada ya makosa kutokea.

Alifafanua kuwa Kamati hizi zinalo jukumu la kuhakikisha kunakuwa na amani na utulivu nchini. Kamati hizi pia zina jukumu la kuchunguza visababishi vya uhalifu unaotishia usalama wa Umma na kuzuia vitendo hivyo.

Alisema matarajio ya Tume na Mahakama ni kuona wadau wa haki wakihamasisha Umma kutumia huduma za Mahakama katika kutatua migogoro yao na pia kuona kamati hizi zikihakikisha usalama kwa Maafisa Mahakama na watumishi wengine kwa ujumla ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa maslahi ya Umma.

Kuhusu uwepo wa kamati za maadili za Mawakili katika ngazi za mikoa, Jaji Kiongozi alisema ni muhimu wananchi wakaelimishwa kuhusu uwepo wa kamati hizo katika mikoa ili wazitumie kuwasilisha malalamiko yao huko badala ya kuyapeleka Makao Makuu ya Mahakama.

Alisema wananchi hawafahamu kuwa katika maeneo yao kuna kamati za maadili ambazo zingeweza kusilkiliza changamorto za maadili ya Mawakili hivyo alikitaka chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kuhakikisha inawaelimisha wananchi uwepo wa kamati hizo na pia kushughulikia maadili ya wanachama wake.

”Tume na Mahakama inatarajia kupungua kwa malalamiko yanayoletwa moja kwa moja Makao Makuu ya Mahakama na badala yake kamati zilizopo mikoani zishughulikie malalamiko hayo”, alisisitiza Dkt. Siyani

Kwa upande wa Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama, Kamishna huyo wa Tume alisema hawa ni wadau muhumu wa Mahakama wanaochakata hatua ya mwisho ya upatikanaji wa haki mahakamani hususan katika mashauri ya madai. Alisema Madalali na Wasambaza nyaraka ndiyo wanaotekeleza amri za Mahakama kwenye mashauri hayo na mipaka yao ya kazi ni mikoa.

Alisema wadau wa utoaji haki hawana budi kuwaelimisha wananchi kuzitumia nafasi za Madalali ili kurahisisha mchakato wa upatikanaji wa haki na pia kuwahamasisha wananchi kujitokeza kufanya kazi hii. Mkoa wa Katavi una Dalali moja tu wakati nchi nzima ina Madalali 118.

Akizungumzia kutenda haki, Jaji Kiongozi amewataka wadau wa utoaji haki nchini kuongozwa na dhamira ya kutenda haki katika kila hatua ya mchakato wa uapatikanaji wa haki.

Alisema Tume na Mahakama inatarajia kuwa wadau wote walio kwenye mnyororo wa utoaji haki wataongozwa na dhamira ya kutenda haki kwa kuwa dhamira hii ikitawala malalamiko kuhusu kutokutendewa haki kwa wananchi yataisha na mashauri yenye ushahidi tu ndiyo yatafikishwa mahakamani hivyo kurahisisha mchakato wa upatikanaji wa haki nchini.

Kamishna alisisitiza kuwa kwa wadau kuongozwa na dhamira ya kutenda haki katika kila hatua kutaimarisha imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama na kwa vyombo vyote vinavyohusika na upatikanaji wa haki nchini.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Dkt. Mustapher Siyani akizungumza jana kwenye Mkutano wa Tume na Wadau wa Utoaji haki Mkoa wa Katavi.

Wadau wa Utoaji haki Mkoa wa Katavi wakiwa kwenye Mkutano kati yao na Tume ya Utumishi wa Mahakama jana mjini Mpanda.

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Utoaji haki Mkoa wa Katavi jana mjini Mpanda.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...