Nihifadhi Abdulla
JESHI LA POLISI ZANZIBAR limezitoa hofu Asasi za Kiraia zinazoendelea kusimamia haki za Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu ZNZ ambapo limesema litaendelea kuhakikishia Haki, Ulinzi na Usalama kwa makundi hayo katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu Mwaka huu 2025 zinalindwa kikamilifu.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Khamis Kombo Khamis alipokuwa akizungumza na wawakilishi wa Asasi za Kiraia zinazotetea haki za Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu zilizofika katika Afisi kuu za Jeshi hilo Ziwani Wilaya ya Mjini Unguja katika kikao maalum cha kujadili mustakbali wa ulinzi na usalama wa makundi hayo wakati wa Uchaguzi.
Aidha Kamishna Khamis ameziasa asasi hizo kufikia pia wadau na taasisi nyengine muhimu nchini ili kwenda sambamba na azma hiyo.
Alizitaja taasisi nyengine kuwa ni pamoja na Vyama vya Siasa, Vikosi vyengine vya Ulinzi na Tume ya Uchaguzi. Alieleza pia kuna haja ya kuwaelimisha wananchi jinsi ya kujiepusha na vitendo vya uvunjaji wa sheria ili kujiweka katika hali ya usalama.
Kamishna amesisitiza pia kuwa Jeshi la polisi lina utaratibu mzuri wa kuwawajibisha maafisa wake pindi wakienda kinyume na utaratibu wa kazi.
Wakizungumza katika kikao wana Asasi hao wameliomba Jeshi hilo kuendelea kuwa msimamizi namba moja wa amani wakati wa uchaguzi sambamba na kuwalinda Wanawake pamoja na Watu wenye Ulemavu ili waweze kuwa salama na kushiriki kikamilifu katika mchakato huo wa kidemokrasia kama wapiga kura, wagombea na mawakala.
Walisema mwaka 2020 baadhi ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu walipatwa na kadhia ya uvunjifu wa haki zao kutoka kwa Vikosi vya Ulinzi na Usalama nchini kama wagombea na mawakala na hivyo kujenga hofu kuhusu ushiriki wao kwa mwaka 2025.
Asasi hizo zimeahidi kuendelea kutoa mashirikiano kwa Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo kwa makundi hayo na kufatilia ushiriki wao katika kipindi hicho cha Uchaguzi Mkuu.
Kikao hicho kilichofanyika Mei 2 huko katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi hilo zimewakutanisha Wawakilishi kutoka Asasi za Kiraia Zanzibar zinazotetea, kulinda na kusimamia haki za Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu zikiwemo Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO) Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Jumuiya inayoshughulika na Changamoto za Vijana Zanzibar (ZAFAYCO) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...