Na Mwandishi Wetu
MKUTANO mkubwa wa uwekezaji utakaowakutanisha wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali kutoka nchi mbalimbali Afrika utafnyika, Pemba, Zanzibar kuanzia Juni 13 mpaka Juni 15 katika viwanja vya uwekezaji, Micheweni, Pemba mwaka huu.
Awali mkutano huo ulipangwa kufanyika Mei 7 mwaka huu lakini waandaaji, Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imetangaza kuusogeza mbele mkutano huo kwa mwezi mmoja kutokana na maombi ya wafanyabiashara wengi.
Akizungumza kutoka Zanzibar, Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA, Saleh Saad Mohamed, alisema pamoja na watu wengi kujiandikisha kushiriki Mkutano huo, bado yapo mapombi mengi ya wafanyabisahara wengine wa ndani na nje ya nchi waliomba kusogeza mbele ili kuwapa nafasi ya kujiandikisha na kuiandaa kushiriki.
"Nichukue fursa hii kuwaomba wafanyabisahara na wananchi kutumia kipindi hiki kujiandikisha kushiriki katika kongamano hili, kwa pamoja tunawaomba mjitokeze kwa wingi kuangalia fursa za uwekezaji Pemba," alisema.
Aidha, alisema ratiba nyingine ya m,kutano huo ipo kama ilivyopangwa ambapo Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi bna kufungua mkutano huo mkubwa wa masuala ya uwekezaji na biashara.
Mkutano huo unaandaliwa na Serikali ya Zanzibar kupitia ZIPA na unatarajiwa kuwakutanisha pamoja watu 1000.
"Hili ni lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutaka kukifungua sasa kisiwa cha Pemba, Zanzibar ni eneo lenye fursa nyingi sana za uwekezaji, wengi wamekuwa wakiifikiria Unguja, lakini zipo fursa nyingi Pemba hususani eneo Micheweni, hii ni fursa kubwa sana kwa wawekezaji," alisema Mohamed.
Alisema kusogeza mbele kwa mwezi mmoja kutatoa fursa ya watu wengi zaidi kushiriki katika mkutano huo.
"Wale ambao bado hawajajiandikisha ni nafasi yao sasa kujiandikisha, muda wa mwezi mmoja unatosha kabisa kwa wale wote wenye nia kushiriki kufanya hivyo," alisema Mohamed.
Aidha, alisema wakati wa Mkutano huo, watapata nafasi ya kuwatembeza wawekezaji na watu watakaohudhuria mkutano kwenye maeneo yote muhimu na yenye fursa ya uwekezaji.
"Kuna maeneo mbalimbali ya uwekezaji, inategemea ni sekta gani unaitaka, Pemba kuna maeneo ya uwekezaji katika uchumi wa buluu kutokana na kuwepo kwa mazao mengi ya bahari, Uwekezaji kwenye sekta ya ujenzi wa nyumba za makazi pamoja na uwekezaji kwenye sekta ya afya, hii yote ni fursa kwa watu kuja kuwekeza," alisema.
Aliyataja maeneo mengine ya uwekezaji kuwa ni kwenye ujenzi wa bandari katika maeneo ya Wete ili kukuza na kuendeleza usafirishaji kwa njia ya bahari, Utalii na ujenzi wa Hoteli.
"Ili kutengeneza mazingira mazuri kwa wawakezaji, Serikali imeanzisha na kuendeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara ili kuunganisha maeneo mbalimbali ya Pemba, na tayari wakandarasi wapo katika maeneo ya miradi," aliongezea kusema.
Kuhusu washiriki wa Mkutano huo, alisema kutokana na kutoa muda zaidi wa kujiandikisha, wanatarajia idadi ya washiriki kuongezeka kutoka kwenye makadilio ya watu 1000 na kuwa zaidi.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...