Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa akifanya mazoezi wakati alipotembelea kituo cha mazoezi katika uzinduzi  kambi ya siku mbili ya uchunguzi wa afya ya moyo iliyofanyika Mei 21, 2025, Dar es Salaam katika Kampasi ya Mloganzila,

Mteknolojia wa Maabara kutoka MUHAS Joseph Temba (wa kwanza kulia) akitoa ufafanuzi kwa Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa wakati alipotembelea kituo cha mazoezi cha chuo hicho kilichopo katikaa Kampasi ya Mloganzila.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu MUHAS Irene Mzokolo (wa kwanza kulia) akitoa ufafanuzi kwa Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa wakati alipotembelea kituo cha mazoezi kilichopo Kampasi ya Mloganzila.
Baadhi ya vifaa vya mazoezi vilivyopo katika Kituo cha mazoezi, Kampasi ya Mloganzila.

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kinatarajia kuanza kutoa mafunzo maalum ya kitaalamu kwa wakufunzi wa mazoezi ya viungo (gym instructors) na wasimamizi wa kumbi za mazoezi (fitness managers),ili kuhakikisha wanakuwa na uwezo wa kuwahudumia wateja wanaopelekwa kufanya mazoezi kwa sababu za kitabibu.

Akizungumza leo Mei21,2025 wakati wa uzinduzi wa kambi ya siku mbili ya uchunguzi wa afya ya moyo bila malipo katika Kampasi ya MUHAS Mloganzila,Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Appolinary Kamuhabwa moja amesema mpango huo unalenga kulinganisha huduma za mazoezi ya viungo ya viwango vya kitaifa vya afya.

“Uzoefu unaonesha kuwa watu wengi huanza mazoezi bila ushauri wa kitabibu, jambo ambalo linaweza kuwa hatari kwa afya hususani moyo,” amesema Profesa Kamuhabwa.

Ameongeza,“Lengo letu ni kuwajengea uwezo waendeshaji wa kumbi za mazoezi ili waweze kutoa huduma kwa kufuata taratibu za kitaalamu za afya,”

Ameonya suala la jamii kufanya mazoezi bila usimamizi wa kitabibu kunaweza kusababisha madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na kupoteza maisha ghafla kwa watu wenye magonjwa ya moyo au matatizo mengine ya kiafya yaliyofichika.

Profesa Kamuhabwa amesema kama sehemu ya mpango huo, MUHAS itazindua kituo kipya cha mazoezi ya viungo mapema wiki hii, ambacho kitakuwa kinatoa vyeti vya mazoezi kama ilivyo kwa dawa zinazotolewa kwa agizo la daktari.

Amesema mafunzo hayo pamoja na uanzishaji wa gym hiyo ni sehemu ya jitihada za kuboresha kiwango cha huduma za mazoezi ya viungo nchini na kupunguza hatari za kiafya kutokana na mazoezi yasiyo na miongozo ya kitaalamu.

Akizungumzia kambi ya uchunguzi inayoendelea, Profesa Kamuhabwa amesema shughuli mbalimbali zinazofanyika kuelekea uzinduzi wa awamu ya pili ya Kituo cha Umahiri cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni pamoja na huduma za magonjwa ya moyo, kinga na tiba kwa wale watabainika kuwa na matatizo ya moyo.

Kwa upande wake, mtaalamu wa fiziolojia Irine Mngolokolo,amesema gym hiyo mpya imeundwa mahsusi kwa ajili ya watu wenye changamoto za kiafya.

Irene ambaye pia ni msaidizi wa kufundisha katika kituo hicho amesisitiza umuhimu wa kuanza mazoezi kwa mpango maalum uliopangwa na mtaalamu, iwe ni ya aerobic au anaerobic, kulingana na mahitaji ya mhusika.

Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Profesa Emmanuel Balandya, amesema kuwa mafunzo ya wataalamu wa afya ya moyo ni moja ya vipaumbele vikuu vya MUHAS.

Kwa sasa, chuo hicho kinatoa programu 93 za kitaalamu, ikiwa ni pamoja na Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Tiba (MSc in Medicine) yenye wanafunzi 20 kila mwaka. Programu nyingine ni ya Tiba ya Moyo ya Watoto (Pediatric Cardiology) na ya Uelewa wa Magonjwa ya Moyo (Cardiovascular Conceptualization) ambazo kila moja huandikisha wanafunzi 10 kwa mwaka.

Ili kukidhi mahitaji ya kitaifa na kikanda, MUHAS pia inandaa programu mpya katika upasuaji wa moyo, usingizi wa ganzi na uuguzi.

Profesa Balandya amesema asilimia 10 ya wagonjwa wanaopata huduma katika vituo hivyo hutokea nje ya Tanzania, jambo linaloonesha mahitaji ya huduma za kitaalamu kikanda.

“Ili kufanikisha malengo yetu ya kitaaluma na huduma za tiba, MUHAS inawekeza kwenye vifaa vya kisasa vya utafiti na ufundishaji, na maandalizi yanaendelea kuanzisha huduma kamili za fiziolojia,”.

mkazi wa Mbagala, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Mtemi Mahunguchira ameishukuru MUHAS kwa mpango huo na kupendekeza kuwa uchunguzi kama huo ufanyike mara kwa mara katika vituo vya afya vya ngazi ya wilaya ili kuimarisha tabia ya kupima afya mara kwa mara.

“Hii ni jitihada muhimu kwetu inapaswa kudumishwa ili hatimaye tuweze kuwa na vituo vya kudumu vya uchunguzi wa afya.”amesema

Mkazi wa Mbezi,Maria Thadeus amesifu ubora wa huduma na kuthibitisha kuwa alipata huduma za kitabibu kwa haraka na kwa ufanisi wakati wa kambi hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...