Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia Afisa Usalama wake wa mkoa wa Ruvuma Jeverino Pembe, limewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda miundombinu ya umeme dhidi ya wizi na uharibifu.
Ametoa wito huo Mei 30, 2025, wakati wa kikao cha kutoa elimu kwa Wazee na viongozi wa Kijiji cha Magwamila Kata ya Lilai Halimashauri ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma kuhusu kuikumbusha jamii umuhimu wa kulinda miundombinu hiyo, akisisitiza kuwa jukumu hilo ni la kila mwananchi kwa ajili ya ustawi wa jamii nzima.
Pembe ameeleza kuwa vitendo vya hujuma dhidi ya miundombinu ya umeme husababisha madhara makubwa yanayowaathiri wananchi wote, amehimiza wananchi kutoa taarifa kuhusu watu wanaohusika na uharibifu huo, huku akieleza kuwa ufichuaji wa wowote na utoaji wa taarifa za uharibifu wa miundombinu una motisha kwa wale watakaosaidia kufichua wahusika.
Ameongeza kuwa uharibifu wa miundombinu ya umeme huleta hasara kubwa kwa shirika na kuchelewesha upatikanaji wa huduma kwa jamii, ameisisitiza jamii kutambua kuwa elimu waliyopewa inapaswa kuwafanya kuwa walinzi wa kwanza wa miundombinu hiyo muhimu.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja kutoka TANESCO Ruvuma, Bw. Alan Njiro, ametoa wito kwa wazee na viongozi wa kijiji cha Magwamila kuhakikisha ujumbe kuhusu madhara ya uharibifu wa miundombinu ya umeme unawafikia wananchi wote, ameonya kuwa vitendo vya kuhujumu miundombinu vinaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo vifo kutokana na mshtuko wa umeme.
Amesema kuwa ni muhimu kwa viongozi wa vijiji kuhamasisha wananchi kuingiza umeme majumbani mwao, hasa baada ya TANESCO kufikisha huduma hiyo katika kijiji cha Magwamila, ameeleza kuwa bado kuna changamoto ya mwamko mdogo wa kuunganisha umeme licha ya uwepo wake, aidha ametoa elimu ya jinsi ya kufanya maombi ya umeme na matarajio ni kuona wananchi wote waliofikiwa na umeme wanaunganisha na kupata huduma hiyo.
Diwani wa Kata ya Lilai Saimon Kapinga amesema wizi wa miundombinu ya TANESCO ni kosa kisheria huku akisisitiza kuwa kesi za uhujumu uchumi hazina dhamana, hivyo wananchi waepuke kujihusisha na vitendo hivyo haramu, Ameagiza mtendaji wa kijiji kuwaandikia barua wakulima ambao mashamba yao yamepitiwa na nguzo za umeme, akiwaagiza kuwa walinzi wa kwanza wa nguzo hizo na kuwajibika endapo kutatokea uharibifu.
Mzee Karume, mkazi wa kijiji cha Magwamila, ameomba TANESCO kuwahamasisha zaidi wananchi wenye mashamba yaliyopitiwa na miundombinu ya umeme ili wawe walinzi wa mali hiyo na kuepuka matukio kama uchomaji wa mashamba yanayoweza kusababisha athari kwenye nguzo za umeme na kusababisha kukatika kwa huduma hiyo muhimu.
Kwa ujumla, TANESCO Ruvuma imesisitiza kuwa ushirikiano kati ya wananchi na shirika hilo ni msingi imara wa kulinda na kuendeleza huduma ya umeme kwa manufaa ya jamii nzima.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...