Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, Sinzo Mgeja,
Na Mwandishi Wetu
KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, Sinzo Mgeja, amewaasa vijana nchini kutokubali kutumika na baadhi ya wanasiasa kuhamasisha uvunjifu wa amani kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, badala yake wawe mstari wa mbele kuilinda.
Sinzo alisema hayo jijini Dar es Salaam, jana, alipozungumza na gazeti hili kuhusu nasaha kwa vijana kuelekea uchaguzi mkuu.
Alisema vijana ndiyo taifa la kesho, hivyo kamwe wasikubali kutumika kama chanzo cha machafuko kwa taifa, badala yake wawe mfano wa kuigwa katika suala zima la kuhubiri amani.
Sinzo alisema jukumu la kulinda amani siyo la mtu mmoja, bali ni la kila Mtanzania wakiwemo vijana ambao ni tegemeo la taifa.
“Tanzania inasifika duniani kuwa ni kisiwa cha amani. Amani hii inapaswa kuendelea kuwepo kizazi hadi kizazi na wanasiasa wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kuilinda amani hiyo,”. alisema.
Sinzo alieleza vijana wanatakiwa kuutanguliza uzalendo na kuachana na baadhi ya wanasiasa hao ambao wanatanguliza maslahi yao binafsi.
Pia, aliwaomba vijana kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi, kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaotokana na CCM akiwemo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani.
“Kwa mujibu wa takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 inaonesha vijana wapo milioni 21. 3 kati ya watu milioni 61. Kutokana na takwimu hizo vijana wana nafasi kubwa ya kuungana pamoja kuwakataa wanasiasa wanaotaka kuwarubuni na kuwashawishi kushiriki katika vitendo visivyofaa kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu," alisema
Kada huyo aliwaomba Watanzania wakiwemo vijana kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu kwa kuwachagua viongozi wanaotokana na CCM.
Sinzo aliwaomba watakaopata fursa ya kuchaguliwa kuwa viongozi kuendelea kuilinda amani na kufanya kazi kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu.
Mbali na hayo, Sinzo aliwaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Dk. Samia na kuhakikisha wanampa kura za kishindo katika uchaguzi mkuu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...