WADAU wa Kilimo katika mnyororo wa thamani wa Mazao ya Mtama na Karanga wameshauriwa kutumia fursa za kiuchumi zilizopo katika Mazao hayo kwa uhakika wa chakula na kujiongezea kipato kwa kaya na Taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa leo Juni 25, 2025 Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo na Utafiti kutoka Wizara ya Kilimo Dkt. Geoffrey Edward katika warsha ya kujadili fursa za kibiashara zilizopo katika mazao yanayovumilia ukame katika nyanda kame husani Mazao ya Karanga na Mtama.
Warsha hiyo ambayo imeandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uboreshaji wa Mahindi na Ngano (CIMMYT) imewakutanisha Wakulima, watafiti, wasindikaji wa Karanga na Mtama, wafanyabiashara pamoja na wakufunzi kutoka vyuo vikuu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa AVISA unaolenga kuongeza tija katika Mazao ya nyanda kame.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt. George Sonda amesema lengo la warsha hiyo ni kubadilishana uzoefu na kuelezana fursa za kibiashara zilizopo katika mnyororo wa thamani wa Mazao hayo.
Akitolea mfano Dkt. Sonda amesema takwimu zinaonesha kuwa uzalishaji wa Mtama ni tani Milioni Moja na laki moja huku mahitaji yakiwa ni tani milioni mbili.
Kwa upande wa zao la Karanga, Dkt, Sonda amesema uzalishaji ni Tani laki tano mia nane themanini na sita hadi Tani laki Saba huku soko la nje uhitaji ni tani elfu ishirini.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...