Wananchi wa Kata ya Matimira, Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, wamepokea kwa furaha ujio wa gari jipya la kubebea wagonjwa lenye thamani ya Shilingi milioni 300, ambalo litatumika kuboresha huduma za rufaa kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.
Wakizungumza baada ya kukabidhiwa gari hilo aina ya Land Cruiser Hard Top, baadhi ya wananchi wamesema ni mara ya kwanza kuona gari la wagonjwa katika kata hiyo, hali inayotoa matumaini makubwa ya kuondoa adha ya usafiri kwa wajawazito na watoto wanaohitaji huduma za haraka za hospitali ya rufaa.
Mzee wa kijiji cha Matimira, Elizia Gerald Komba, amesema hajawahi kushuhudia serikali kupeleka gari la wagonjwa katika eneo hilo tangu kuzaliwa kwake.
Aliongeza kuwa ujio wa gari hilo ni mkombozi mkubwa kwa jamii ya Matimira, hasa kwa wagonjwa waliokuwa wakihangaika kufika hospitali kwa muda mrefu.
Naye Agnetha Gerold Nyoni, mkazi wa kata hiyo, amesema wanawake wengi wamekuwa wakijifungulia njiani kutokana na kukosekana kwa usafiri wa haraka, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Diwani na Mbunge kwa kufanikisha upatikanaji wa gari hilo, akisema hatua hiyo itasaidia mama na mtoto kuwa salama wakati wa kujifungua.
Akizungumza wakati wa makabidhiano Katibu wa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Nassa Sanga, amesema gari hilo lilipokelewa rasmi tarehe 26 Mei 2025 kutoka Wizara ya Afya, huku akiwataka wananchi kuhakikisha gari hilo linatumiwa kwa kusudi la kusafirisha wajawazito na watoto, na si shughuli nyingine.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Matimira ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Menance Komba, amewahakikishia wananchi kuwa gari hilo litatumiwa kwa usafiri wa wagonjwa pekee, na si kubebea mizigo kama mkaa au mchanga, amesema litahudumia kila mtu bila ubaguzi na watalihifadhi kwa uangalifu mkubwa.
Wananchi wa Matimira wameeleza kuwa wanathamini jitihada za serikali ya awamu ya sita katika kuboresha huduma za afya vijijini, na wanatarajia kwamba maboresho hayo yataendelea ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya bila kikwazo cha usafiri.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...