Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Ngerengere
MGOMBEA Urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ametoa ahadi kwa wakulima kuwa Serikali itajenga vituo vya zana za kilimo maeneo mbalimbali nchini ambavyo vitakavyotoa huduma za ukodishaji zana hizo ikiwemo matrekta kwa gharama nafuu.
Amefafanua kuwa hivi sasa wakulima nchini wamekuwa wakipata changamoto ya kukodishiwa matrekta kwa gharama kubwa, hivyo kupitia mpango huo watakodisha zana hizo kwa nusu ya bei wanayotozwa sasa na watu binafsi.
Mgombea Urais wa CCM Dk.Samia Suluhu Hassan akiwa katika mkutano wa kuomba kura kwa mamia ya wananchi wa Kata ya Ngerengere katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro vijijini mkoani Morogoro ameeleza hatua ambazo atachukua baada ya kuchaguliwa katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu na ahadi yake kwa wakulima ni kuendelea kuboresha mazingira ya sekta ya kilimo.
Dk.Samia amewaleza wananchi waliokuwa wakimsikiliza kwamba Serikali itajenga vituo viwili vya ukodishaji zana za kilimo hivyo wakulima nchini watakodisha matrekta kwa nusu ya bei ambayo itakuwa tofauti na bei ambayo wanatozwa watu binafsi ambayo ni kubwa.
Pia amesema mbali na wakulima kupatiwa ruzuku ya mbolea, serikali imeanzisha kituo cha uzalishaji miche ya chikichi ambapo hadi sasa miche zaidi ya 82,000 imegawiwa bure kwa wakulima.
Pamoja na mambo mengine pia ameahdi Serikali kujenga maghala mawili ya kuhifadhia mazao na katika kutekelezwa ahadi hiyo ameilekeza Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Kilimo, kujenga ghala la kuhifadhia mazao katika kituo cha reli ya SGR.
“Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na halmashauri watoe eneo. Hii itakuwa sehemu mojawapo ya ushoroba wa viwanda ambao utachochea ukuaji uchumi katika eneo hili," amefafanua Dk.Samia alipokuwa akizungumza n wananchi wa Ngerengere.
Aidha amesema kwamba Serikali pia imetoa pikipiki 68 kwa maofisa ugani na vipima udongo katika Halmashauri ya Wilaya hiyo huku akieleza wamejenga maghala matatu ambayo kabla ya hapo wilaya hiyo haikuwa na maghala ya kuhifadhia chakula.
Kuhusu wakulima wa mazao ya ufuta, mbaazi na korosho Dk.Samia amesema wamenufaika kupitia uuzaji mazao hayo kwa mfumo wa stakabadhi ghalani na kuingiza zaidi ya sh. bilioni 11.
Akiizungumzia sekta ya mifugo katika Wilaya hiyo Dk.Samia amesema itajengewa mashamba darasa 15 kwa ajili ya malisho na uzalishaji mifugo.Pia Serikali akiahidi Serikali kutoa Sh.bilioni 2.3 za mikopo kwa wajasiriamali 7,015 kupitia halmashauri.
Kwa upande wa usambazaji nishati ya umeme vijijini, amesema vijiji 149 na vitongoji 417 vimefikishiwa huduma hiyo kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Katika ahadi yake kwa wananchi hao pia Rais Dk.Samia amesema Serikali itajenga barabara ya Bigwa-Kisaki kwa kiwango cha lami na ahadi hiyo ameitoa baada ya mgombea ubunge Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Hamisi Taletale maarufu Babu Tale kutoa ombi kwa Rais kuhusu Ujenzi wa barabara hiyo.
Hata hivyo mgombea wa CCM Dk.Samia amewaomba wananchi hao kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu ambapo amewaambia katika fomu ya kugombea kutakuwa na picha yake ikiwaangalia.
“Niwaombe wananchi siku ya kupiga kura mkakipigie Chama Cha Mapinduzi,mkanipigie mimi,Wabunge na madiwani wa CCM,wale jamaa zangu wameweka mpira kwapani…”
Akizungumza na viongozi wa CCM katika nafasi mbalimbali za uongozi amesema Chama kimewapa vitendea kazi kama baiskeli na pikipiki hivyo wavitumie katika kwenda kwa wananchi kuomba kura za wagombea wa Chama hicho.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...