
.jpeg)
Na Karama Kenyunko, Dar es Salaam
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imevitaka vyombo vya habari nchini kutumia kalamu zao kwa busara kwa kuepuka kuripoti taarifa zenye maudhui ya chuki, mgawanyiko au uchochezi wa vurugu wakati wa kipindi cha kuelekea na wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Wito huo umetolewa leo Agosti 04, 2025 na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhani Kailima wakati wa ufunguzi rasmi wa mafunzo kwa wahariri na waandishi wa habari kuhusu uchaguzi huo, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kailima alisisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kulinda amani na mshikamano wa kitaifa, na kwamba taarifa zinazotolewa zinapaswa kujenga umoja wa kitaifa badala ya kusababisha taharuki kwa jamii.
"Tunatarajia kuona habari za uchaguzi zikitolewa kwa usahihi na kuepuka upotoshaji. Mzingatie maadili ya uandishi wa habari na mchuje maudhui yanayoweza kuchochea chuki au ghasia," alisema Kailima.
Aidha, aliwataka waandishi na wahariri kuzingatia uwazi na usawa katika uandishi wa habari za uchaguzi huku wakiepuka upendeleo wowote, akisisitiza umuhimu wa kusambaza taarifa rasmi na zilizothibitishwa hasa kupitia mitandao ya kijamii.
Katika hotuba hiyo, Kailima pia alieleza kuwa Tume inatarajia kuendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vya habari kupitia vipindi vya redio, televisheni na majukwaa mengine, kwa lengo la kutoa taarifa sahihi kwa wakati na kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.
Akizungumzia ratiba ya uchaguzi, Kailima alifafanua kuwa utoaji wa fomu kwa wagombea wa Urais na Makamu wa Rais utafanyika kuanzia tarehe 09 hadi 27 Agosti, 2025, na uchaguzi wenyewe utafanyika siku ya Jumatano, tarehe 29 Oktoba, 2025.
Vilevile, aliwaeleza washiriki kuwa Tume tayari imetunga sheria, kanuni, miongozo na maelekezo kwa ajili ya uchaguzi huo, na kwamba nakala za nyaraka hizo zitagawiwa kwa waandishi ili kuwasaidia kuzingatia matakwa ya kisheria katika kazi zao.
Katika hatua nyingine, Tume imetangaza kuwa kuanzia tarehe 01 hadi 30 Septemba, 2025, itakuwa na mfumo rasmi wa usajili wa vyombo vya habari na waandishi, ambapo kila chombo kitaorodhesha majina ya waandishi wake pamoja na maeneo ya kazi watakayokuwa wakiripoti siku ya uchaguzi, kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho maalum.
Kailima alihitimisha hotuba yake kwa kuwashauri washiriki wa mafunzo hayo kutumia fursa hiyo kujifunza kwa makini, kuuliza maswali na kushirikiana katika kuhakikisha taarifa sahihi na zenye tija zinawafikia wananchi wote, akisisitiza kaulimbiu ya mwaka huu kuwa:
“KURA YAKO, HAKI YAKO – JITOKEZE KUPIGA KURA.”
Mafunzo hayo yamelenga kuwaandaa wanahabari kuelewa sheria, mchakato wa uchaguzi, maadili ya taaluma, ulinzi wa taarifa binafsi na namna bora ya kuripoti migogoro na majanga katika kipindi cha uchaguzi.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura, Giveness Aswile akizungumza katika Mkutano wa Tume, Wahariri na Waandishi wa Habari, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, Agosti 4, 2025.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhani Kailima (Kulia), akimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura, Giveness Aswile, kabla hajafungua Mafunzo ya Wahariri na Waandishi wa Habari, yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, leo Agosti 4, 2025.
Picha na INEC.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhani Kailima (Katikati waliokaa), Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura, Giveness Aswile (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Daftari na TEHAMA, Stanslaus Mwita (kushoto), Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria Selemani Mtibora (wa pili kulia), na Mwenyekiti wa Mafunzo ya Wahariri na Waandishi wa Habari, Lilian Timbuka (kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahariri na waandishi wa habari baada ya kufunguliwa kwa mafunzo hayo katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, leo Agosti 4, 2025.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...