
Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv
DUNIA inavyoelekea katika maadhimisho ya Siku ya Uzazi wa Mpango Duniani Septemba 26, mjadala kuhusu umuhimu wa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana umeibua hisia kubwa nchini. Shirika la Marie Stopes Tanzania, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na wadau mbalimbali, limeendesha kampeni ya kutoa elimu ya afya ya uzazi na kijinsia kwa wanafunzi wa shule na vyuo jijini Dodoma
Akitoa elimu hiyo Dkt. Lerise Mashingo, mtaalamu kutoka Marie Stopes, amesema vijana ni kundi muhimu na lenye mchango mkubwa kwa taifa.
“Vijana wanashika asilimia kubwa ya Watanzania, na wao ndio rasilimali muhimu ya taifa letu. Lakini changamoto tulizonazo ni kubwa takwimu za mwaka 2022 zinaonyesha kuwa binti mmoja kati ya wanne tayari alikuwa amepata ujauzito akiwa na umri wa miaka 15–19. Hili linaonesha hitaji la dharura la kuwekeza kwenye elimu ya afya ya uzazi,” amesema.
Amefafanua kuwa elimu ya afya ya uzazi haihusu tu njia za kupanga uzazi, bali pia afya ya mwili, kinga dhidi ya magonjwa ya zinaa, lishe, na mbinu za kujikinga na unyanyasaji wa kijinsia. Kupitia mafunzo hayo, vijana hupata nafasi ya kuuliza maswali moja kwa moja kwa wataalamu na hivyo kuongeza uelewa.
“Vijana wengi hufundishwa darasani juu ya uzazi wa mpango bila kuona zana husika. Tulipowaletea vielelezo na kuonyesha kitanzi au kijiti, waliweza kupata picha halisi na kuondoa hofu na dhana potofu,” amesema Dkt. Mashingo.
Hata hivyo, amekiri kuwa kuzungumza waziwazi na vijana kuhusu masuala ya uzazi bado si rahisi kwa sababu ya mila na desturi.
“Lakini vijana wanahitaji kupata taarifa kutoka kwa mtu anayeeleweka na wanayemuamini. Wakihisi tunawaficha ukweli, hupoteza imani na kwenda kutafuta taarifa kwingine ambako mara nyingi si salama,” amesema.
Ameongeza kuwa changamoto kubwa ni namna ya kuanzisha mazungumzo hayo, lakini pindi mazingira ya kuaminiana yanapojengwa, vijana huwa huru kuuliza maswali.
Dkt. Mashingo ametoa wito kwa wazazi na walezi kuzungumza na vijana kwa lugha rahisi na ya heshima na waepuke kauli zinazokandamiza kama “vijana wa siku hizi...”
Lakini pia wawe tayari kujibu maswali ya watoto kwa ukweli au kumpeleka mtoto kwa mtaalamu iwapo hawana majibu sahihi na waelewe kuwa muda sahihi wa mazungumzo ni pale mtoto anapouliza swali husika.
“Wazazi wengi hudhani kuficha ukweli ni njia ya kuwalinda watoto, kumbe matokeo yake ni mabaya zaidi. Mtoto akikuchukulia kama muongo, hatakuuliza tena,” amesema.

Eric Asenga, Meneja wa Biashara wa Marie Stopes Tanzania, amesisitiza umuhimu wa kondomu kama njia rahisi na salama zaidi ya kujikinga.
“Kondomu zinapatikana kwa urahisi. Kwa mwaka tunasambaza zaidi ya vipande milioni 8 vya Life Guard nchini. Mbali na kupanga uzazi, hulinda dhidi ya magonjwa ya zinaa ikiwemo VVU,” amesema.
Ameeleza kuwa tofauti ya Life Guard ni uwepo wa vionjo vinavyoongeza msisimko kwa wapenzi, jambo linalochangia kuondoa malalamiko kwamba zinapunguza ladha ya tendo.
Zaidi ya usambazaji, Asenga amesema shirika linaendesha elimu ya matumizi sahihi kupitia shule, vyuo na mikusanyiko ya vijana.
Rebeca, mwanafunzi wa kudato cha nne kutoka shule ya Sekondari Kisasa aliyehudhuria elimu hiyo, amesema.
“Tumejifunza siyo tu kuhusu njia za uzazi wa mpango, bali pia namna ya kujikinga na ukatili wa kijinsia na haki zetu. Kwa umri wetu, tumeelezwa njia salama zaidi ni kutokujihusisha na mapenzi. Hii imetufundisha kupanga ndoto zetu kwa utulivu.”
Dkt. Mashingo amehitimisha kwa kutoa wito kwa jamii kushirikiana katika kutoa elimu kwa vijana:
“Hili si jukumu la serikali au mashirika pekee."
Kila mzazi, mlezi na mwalimu ana nafasi yake. Tusipoweka elimu sahihi kwa vijana, wataenda kutafuta majibu kwa vyanzo visivyofaa na matokeo yake yatakuwa mabaya.
Kadri Tanzania inavyojiandaa kuadhimisha Siku ya Uzazi wa Mpango Duniani, ujumbe kwa Watanzania ni mmoja: Elimu sahihi ya afya ya uzazi kwa vijana ni kinga ya mustakabali wa taifa. Kupitia elimu hii, vijana hufanya maamuzi bora, kuepuka mimba za utotoni, kujikinga na magonjwa ya zinaa na kulinda ndoto zao.
“Changamoto zipo, lakini fursa pia ni kubwa. Vijana wakipata taarifa sahihi mapema, watakuwa kizazi chenye uelewa, afya bora na mustakabali thabiti.”
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...