Wafanyakazi katika kiwanda cha kuchakata viungo Cha Horizon Group wakitayarisha mazao hayo katika mji wa Kaduna. Nigeria. Wakulima wa Viungo nchini Tanzania, Nigeria na Madagascar watanufaika na mipango kabambe wa maboresho ya mazao hayo ili kukidhi viwango vya kimataifa na kukuza mauzo.
WAKULIMA wa mazao ya viungo Tanzania wamepata neema mpya kufuatia uamuzi wa kampuni ya Aavishkaar Capital kuwekeza Dola za Marekani milioni 5 kwa ajili ya ukuzaji na uchakataji wa mazao hayo ili kukidhi mahitaji ya soko.
Fedha hizo zitawasaidia wakulima zaidi ya 3,000 katika nchi za Tanzania, Nigeria na Madagascar kupitia kampuni ya Horizon Group inayofanya kazi na wakulima wa viungo.
Aavishkaar, inayofanya kazi chini ya mwamvuli wa Aavishkaar Group, imetangaza uwekezaji huo barani Africa kwa kushirikiana na Benki ya Uwekezaji na Maendeleo inayomilikiwa na Serikali ya Ujerumani, KfW.
Uwekezaji huo umewezeshwa na Mfuko wa Dunia wa Kusaidia Mnyororo wa Ugavi (GSCSF) ambao ilitoa mkopo wa Dola za Marekani milioni 5 kwa Horizon Group Africa. Huu ni uwekezaji mkubwa wa nne kufanywa na GSCSF barani Afrika.
Kampuni ya Horizon Group hujihusisha na utafufutaji na uchakataji wa viungo na kuviuza katika nchi za Umoja wa Ulaya (EU), Asia na Marekani. Kampuni hiyo inafanya kazi kupitia vituo vyake nchini Tanzania, Nigeria na Madagascar, ikinunua na kusaidia katika uzalishaji na uchakataji wa tangawizi, bizari (manjano), iliki, mdalasini, karafuu na pilipili manga.
Mkopo huo utaelekezwa zaidi katika kukuza mtaji wa Horizon Group, hususan katika ununuzi wa malighafi ili kukidhi viwango na mahitaji wa soko la kimataifa.
Kampuni ya Horizon Group ilianzishwa nchini Nigeria mwaka 2006 ikijihusisha na biashara ya mazao mbali mbali ya kilimo, vyakula vya kusindika na Samani. Mwaka 2017, kampuni hiyo iliamua kujikita katika kutafuta, kuchakata na kusafirisha viungo kutoka katika nchi za Tanzania, Nigeria na Madagascar zinazoongoza kwa uzalishaji wa mazao hayo.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba nchi hizi zina faida ya kuwa na nguvu katika ushindani wa soko la viungo kama vile tangawizi, iliki, mdalasini, karafuu, bizari (manjano) na pilipili manga kwa kuwa na hali ya hewa na udongo unaoruhusu kilimo cha viungo. Kihistoria, zimekuwa pia miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa viungo.
Kampuni hiyo inajihusisha na uchakataji wa viungo vya ogani na vile vinavyozalishwa kwa kutumia mbolea za kisasa, dawa za kukuzia na kuulia wadudu. Kuongezeka kwa uelewa wa watu na kukua kwa mahitaji ya vyakula vya ogani duniani vimesaidia kukua kwa soko la viungo vya ogani, hivyo kuiwezesha Horizon Group kupata bei bora na faida.
Horizon ina uhusiano wa moja kwa moja na wakulima zaidi ta 3,000 huku ikifanya uangalizi mkubwa kwenye uendeshaji wa shughuli zao za kilimo. Kampuni hiyo huwapatia wakulima mafunzo ya mbinu bora za kukuza kilimo cha ogani. Zaidi ya hayo, imefanikiwa kuwaunganisha wakulima katika vikundi vya ushirika ili kuhakikisha na kuwezesha kupata ithibati ya ogani na ufuatiliaji kamili.
“Tunafurahi kufanya kazi na Aavishkaar Capital tunapoanza awamu nyingine ya safari yetu ya kukua. Uzoefu wao katika kukuza biashara, kuimarisha mifumo ya uongozi, kuwezesha upatikanaji wa soko, na kufungua mitaji utakuwa wa manufaa tunapoijenga Horizon kuwa kampuni inayoongoza katika uchakataji wa viungo,” alisema Jomy Antony, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Horizon Group.
Akitoa maoni yake kuhusu uwekezaji huo, Darren Lobo, mkurugenzi katika kampuni ya Aavishkaar Capiital, alisema: “Tumefurahi kufanya kazi na timu ya kipekee ya Horizon Group, ambayo inaleta uzoefu wa zaidi ya miaka 80 ya utaalamu katika uzalishaji na uuzaji wa viungo, ili kujenga moja ya kampuni kubwa ya kuchakata viungo Afrika.”
“Kiongozi wa Divisheni katika benki ya KfW, Dr Markus Aschendorf, aliongeza: Uwekezaji wetu katika Horizon Group kupitia Mfuko wa Dunia wa kusaidia Mnyororo wa Ugavi (GSCSF) unaakisi dhamira yetu ya kuimarisha mnyororo endelevu wa ugavi Afrika na Asia. Tunaamini kwamba mtaji unaotumika kwa lengo utachochea uwekezaji unaozingatia masuala ya mazingira, jamii na uongozi huku ukifungua ukuaji shirikishi. “
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...