*Aweka wazi mpango wa kumaliza msongamano wa malori Tunduma mkoani Songwe
*Agusia maboresho reli ya TAZARA,maegesho ya kisasa kuepusha malori barabarani
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Tunduma
NI maelfu ya wananchi,ni maelfu ya wananchi, ni maelfu ya wananchi ! Hivyo ndivyo unavyoweza kuelezea maelfu ya wananchi wa Tunduma katika Mkoa wa Songwe wamejitokeza kwa wingi katika mkutano wa kampeni za mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na maelfu ya wananchi katika Uwanja wa Shule ya Msingi Tunduma mkoani Songwe leo Septemba 3,2025 , Mgombea Urais wa CCM ,Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano wake huku akitumia nafasi hiyo kuelezea hatua mbalimbali ambazo Serikali anayokwenda kujiunga baada ya Uchaguzi mkuu itafanya kwa ajili ya kuleta maendeleo.
Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ametumia mkutano huo wa Tunduma kuelezea mpango wa Serikali wa kuboresha miundombinu ya TANZAM inayounganisha Tanzania na Zambia katika Mkoa wa Songwe pamoja na maboresho ya reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) lengo likiwa kumaliza msongamano wa maroli yanayokwenda nchini Zambia kupitia mpaka wa Tunduma.
Ameeleza kuwa tayari ujenzi wa barabara hiyo imeanza kujengwa kwa njia nne kutoka Igawa hadi Tunduma kwa urefu wa kilometa 75 hatua ambayo itaimarisha shughuli za usafirishaji mizigo katika njia hiyo.
“Maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam imechochea ongezeko la mizigo kutoka tani milioni 15 hadi tani milioni 28 kwa mwaka. Natambua maboresho makubwa yaliyofanyaka Bandari ya Dar es Salaam yameonegza mizigo inayotoka nchini kwenda nje ya nchi.
“Kabla ya maborseho tani za mizigo iliyokuwa ikiingia bandarini likuwa milioni 15.8 lakini baada ya maboresho bandari inapokea tani milioni 28.Mzigo unaovuka mpaka wa Tunduma umepanda kutoka tani milioni 3.7 hadi tani milioni tisa.
“Hali hiyo inaleta msongamano wa maroli ya mizigo yanayoelekea kuvuka mpaka wa Tunduma, kwa maana hiyo tumeanza ukarabati kwa kupanua barabara kuu ya TANZAM inayounganisha Zambia na Tanzania. Kazi inaendelea na tutaendelea nayo mpaka itakapokamilika,”amesema Rais Dk.Samia.
Kuhusu maboresho ya reli ya TAZARA amesema kuwa reli hiyo ni muda mrefu hivyo imechoka na kusababisha kubeba kiwango kidogo cha mizigo wakati huu ambao idadi ya mizigo ikiongezeka katika Bandari ya Dar es Salaam.
Pia ameahidi katika kipindi cha miaka mitano ijayo Serikali itakamilisha ujenzi wa bandari kavu eneo la ekari 1,800 katika Kata ya Mpemba ili maroli yasipaki barabarani.Pia wataongeza barabara ya mbadala itakayoanzia Mwakabanga.
“Tutajenga maegesho ya kisasa, kuongeza mizani, kuharakisha uchakataji nyaraka kabla ya magari kufika mpakani. Pia, serikali tumeanza kuzungumza na mamlaka za ukusanyaji mapato Zambia zifanyekazi saa 24 kama ilivyo kwa Tanzania," amesema Dk.Samia Suluhu Hassan .
Ameongeza Serikali imejipanga kutekeleza mradi wa umeme kutoka Iringa - Njombe hadi Tunduma yenye msongo wa kilovoti 730 kati ya hizo kilovoti 400 zitatumika Tunduma na Rukwa huku kilovoti 330 zitakwenda kuuzwa nchini Zambia.
Amesisitiza kuwa wamekamilisha mazungumzo, na wameanza mchakato kujenga njia hiyo ili umeme ufike kwa uhakika. Hiyo inakwenda sambamba na uhamasishaji matumizi ya nishati safi kwa sababu umeme pamoja na gesi ni nishati safi.
Pamoja na hayo Rais Dk.Samia amewaahidi wananchi wa Tunduma kuwa miaka mitano ijayo Serikali itafanya mambo makubwa zaidi katika sekta ya elimu, afya, maji na umeme.
“Tunakwenda kutoa huduma kwa wananchi, tutaendelea kuongeza shule, elimu bila ada, mikopo kwa wanafunzi wa vyuo na VETA, kujenga vyuo vya VETA kuwawezesha vijana wapate ujuzi na kujiajiri.
“Tutaendelea kujenga vituo vya afya na zahanati, tunakwenda kumaliza miradi ya maji lengo kuhakikisha kila Mtanzania apate maji safi na salama kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini. Baadhi ya maeneo tumefikia lakini baadhi ya maeneo miradi inaendelea. “
Katika hatua nyingine Rais Dk.Samia amesema alipokuwa anatoa ahadi kwa mambo atakayoyatekeleza katika siku 100 za mwanzo katika Serikali aliahidi kuanza kwa mpango wa bima ya afya kwa wote utakaoanza kwa majaribio ambapo Amefafanua wagonjwa watakaopata wa vipimo vya matibabu ni wale ambao watabainika kutokuwa na uwezo.
Ametumia nafasi hiyo pia kuomba kura kwa wananchi katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu na kuwasisitiza wachague mafiga matatu kwa kuanza na Rais ,Mbunge na madiwani ili kazı ya kuleta maendeleo kwa Watanzania iendel e.
Amesema kauli mbiu ya CCM inasema Kazi na Utu wanasonga mbele ambapo amesema kwamba Chama hicho kinafanya kazi na kujali utu.” Tunafanya kazi nakujali utu wa mtu na ndiyo maana tunasema 'Kazi na Utu' kuanzia huduma za afya, maji ni kujali utu wa mtu.
“Tunaongeza uzalishaji chakula ni kujali utu wa mtu. lakini la pili tunajiamini, uwezo tunao na nyezo za kufanyiakazi tunazo. Hivyo niwaombe wananchi pigeni kura kwa CCM kama kawaida yetu ni mafiga matatu.”
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...