WANANCHI wa Afrika Mashariki, kupitia Bunge la Afrika Mashariki (EALA), leo wametoa salamu za rambirambi na heshima kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Mheshimiwa Raila Amolo Odinga, aliyefariki dunia jana nchini India.

Wabunge hao walitumia kikao hicho maalum si tu kumlilia, bali pia kusherehekea maisha yake, wakimtambua kama mwana wa Afrika Mashariki, kiongozi shupavu aliyepigania demokrasia, haki za binadamu na umoja wa eneo hili.

Akizungumza wakati wa kujadili hoja hiyo, Mbunge wa Afrika Mashariki kutoka Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Abdullah Hasnu Makame, alieleza kwa hisia ukaribu mkubwa uliokuwapo kati ya Marehemu Raila Odinga na Tanzania.

Dkt. Makame alitaja mambo manne muhimu yanayodhihirisha undugu huo:
1. Simulizi ya kihistoria ya Raila na kaka yake Oburu Odinga, ambao waliwahi kutumia pasi za kusafiria za iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika, na baadaye za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ishara ya udugu wa kweli wa Kiafrika.
2. Uhusiano wa karibu kati ya Raila Odinga na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, urafiki uliokuwa wa kuheshimiana na kuaminiana.

3. Mapenzi ya Raila kwa Watanzania, yaliyodhihirika wazi alipohudhuria harusi ya Mtanzania Edwin Odemba tarehe 29 Juni mwaka huu, akionyesha unyenyekevu na upendo wa kweli kwa watu wa kawaida.

4. Mapumziko yake visiwani Zanzibar baada ya kushindwa kutangazwa mshindi katika uchaguzi mkuu wa Kenya, hatua iliyompa nafasi ya kutafakari, kupumzika, na kuandika upya ukurasa wa maisha yake ya kisiasa.

Dkt. Makame alisisitiza kuwa mchango wa Raila katika uongozi, ubinadamu na utu utabaki kuwa sehemu ya kumbukumbu za vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa maneno yake, “Raila hakuwa kiongozi wa Kenya pekee, bali alikuwa alama ya matumaini na uthubutu wa Afrika Mashariki yote.”

Bunge la Afrika Mashariki lilikubaliana kwa pamoja kwamba maisha ya Raila Odinga yabaki kuwa somo kwa viongozi wa sasa na wa baadaye, kwamba siasa inaweza kuwa chombo cha kuhudumia watu — si cha kugombania madaraka.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...