Kigali, Rwanda – Oktoba 24, 2025:
Airtel Africa Foundation imeingia katika ushirikiano wa pamoja na Shirika la Kimataifa la Mawasiliano (ITU), Mamlaka ya Jamii ya Habari ya Rwanda (RISA), na Cisco katika kujenga uwezo na kukuza ujuzi wa kidijitali, chini ya Mpango wa Vituo vya Mabadiliko ya Kidijitali (Digital Transformation Centres – DTC).
Ushirikiano huu unalenga kupunguza pengo la kidijitali na kuhamasisha ujumuishi wa kidijitali kwa kutoa huduma ya intaneti bila malipo na mafunzo ya ujuzi wa kidijitali kwa jamii zisizohudumiwa ipasavyo nchini Rwanda, katika kuendana na utekelezaji wa Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030.
ITU itatoa maudhui ya mafunzo ya ujuzi wa kidijitali kwa vituo vya DTC chini ya mpango huo, pamoja na shughuli nyingine za kikanda za kujenga uwezo. Aidha, ITU itarahisisha fursa za mitandao ya ushirikiano kwa ajili ya kukuza uelewa na ujumuishi wa kidijitali, ambazo zitaruhusu upatikanaji wa utaalamu na mbinu bora.
Akizungumza na waandishi wa habari, Bw. Sujay Chakrabarti, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Rwanda alisema:
"Ushirikiano wa leo kati ya Airtel Africa Foundation, ITU, RISA na Cisco ni hatua muhimu katika kupunguza pengo la kidijitali na kuwawezesha vijana wa Rwanda kupata ujuzi wa kidijitali. Ushirikiano huu unaonyesha nguvu ya ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na mashirika ya kimataifa katika kuiwezesha jamii."
Airtel Africa Foundation, kupitia Airtel Rwanda, itaviwezesha vituo vya DTC kwa kuwapatia vifaa vya maunganisho ya mtandao (routers), Wi-Fi na vifurushi vya data bila gharama, kuhakikisha utekelezaji mzuri wa mafunzo na upatikanaji wa majukwaa ya elimu ya kidijitali.
Ushirikiano huu wa kihistoria unaendana na dhamira ya Rwanda kuwa uchumi unaotegemea maarifa na unasaidia programu za kitaifa kama Connect Rwanda zinazohamasisha upatikanaji wa simu janja na huduma za kidijitali kwa jamii zisizohudumiwa.
Bi. Esi Asare Prah, Mkuu wa Programu wa Airtel Africa Foundation akimwakilisha Dk. Segun Ogunsanya, Mwenyekiti wa Airtel Africa Foundation alisema:
"Ushirikiano huu unaonyesha dhamira yetu ya kusaidia malengo ya maendeleo ya kitaifa na kupunguza pengo la kidijitali kupitia ushirikiano wenye tija. Tumefurahi kushirikiana na ITU kutekeleza maono haya na kuchangia safari ya Rwanda kuwa jamii yenye uwezo wa kidijitali."
Dk. Emmanuel Mannaseh, Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Kimataifa la Mawasiliano (ITU) alisema:
"Ushirikiano wetu na Airtel Africa Foundation unaanza hapa Rwanda, tukilenga kuimarisha ujuzi wa kidijitali katika jamii zisizohudumiwa ili kukuza muunganisho. Mpango huu unaweka msingi wa ushirikiano mpana katika kanda, tukiwa na lengo la kupanua kazi hii katika Vituo vingine vya Mabadiliko ya Kidijitali barani Afrika."
Bw. Antoine Sebera, Mtendaji Mkuu wa RISA alisema:
"Tunachoshuhudia leo ni ushirikiano kwa vitendo. Takwimu zinaonyesha kuwa watu milioni 900 barani Afrika bado hawajaunganishwa na mtandao, hivyo juhudi za ziada zinahitajika kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma. Hii inaipa Rwanda nafasi ya mbele kwa kuweka mkazo katika kuwawezesha vijana. Vituo hivi vitakuwa na mchango mkubwa katika kuwaelimisha vijana kutumia teknolojia kama AI. Mabadiliko ya Kidijitali ndiyo yanayoiongoza dunia leo, na Afrika wala Rwanda haiwezi kubaki nyuma."



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...