Nahodha msaidizi wa timu ya soka ya Kilimanjaro FF inayomilikiwa na Watanzania nchini Sweden, Richard Ntirugelegwa maarufu kama Messy, akimkabidhi Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, kombe la ushindi wa michuano ya Bonanza la Serengeti iliyofanyika nchini Ubelgiji mwezi Agosti 2025. Tukio hilo lilifanyika tarehe 25 Oktoba, 2025, katika makazi ya balozi jijini Stockholm.
TIMU ya Kilimanjaro FF inayomilikiwa na kuendeshwa na Watanzania waishio nchini Sweden imeshika nafasi ya tatu katika ligi ya daraja la sita kwenye jiji la Stockholm katika msimu wa 2024/25 iliyohitimishwa mwezi Oktoba.
Akimtaarifu Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, wakati wa hafla fupi nyumbani kwa balozi ya kulikabidhi kombe la ushindi wa Bonanza la Serengeti, Mwenyekiti wa Kilimanjaro, Norman Jasson, alisema mwakani wamepania kushika nafasi ya kwanza au ya pili ili waingie daraja la tano.
Mhe. Balozi Matinyi aliwapongeza wachezaji wa Kilimanjaro na kuwataarifu kwamba Ubalozi unaitafutia wadhamini kutoka nyumbani Tanzania ili mbali ya kucheza soka, timu hiyo pia ilitangaze vema jina la Tanzania na fursa zilizopo nchini katika uwekezaji, biashara na utalii.
Vilevile, Mhe. Balozi Matinyi aliwaambia wachezaji na uongozi wa Kilimanjaro kwamba mipango inaendelea kwa kushirikiana na mamlaka za michezo nchini ili ikifanikiwa basi wachezaji vijana wa Tanzania waje nchini Sweden kuiongezea nguvu Kilimanjaro na pia kuwapa uzoefu wa kucheza Ulaya na pengine kubakia katika timu za Ulaya.
Kwa mwaka huu timu za Stocksunds IF na IFK Lidingö BK ndizo zimeshika nafasi za juu na hivyo kupanda daraja. Mfumo wa michuano ya soka nchini Sweden una madaraja saba kuanzia ngazi za miji.
Katika hafla hiyo iliyofanyika kabla ya tukio la kuangalia mechi ya Yanga na Silver Striker kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, nahodha wa Kilimanjaro, Richard Ntirugererwa, maarufu kama Messy, alimkabidhi Mhe. Balozi kombe la Bonanza la Serengeti ambalo ililitwaa mwezi Agosti nchini Ubelgiji kwa mara ya nne mfululizo.
Timu ya Kilimanjaro leo Jumapili tarehe 26 Oktoba, 2025, inaendelea na raundi ya pili ya michuano ya mtoano ya Kombe la Stockholm ambapo mshindi wake atashiriki kwenye michuano ya Chama cha Soka cha Sweden (SFF).
Ubalozi wa Tanzania, Stockholm, Sweden.
Jumapili, Oktoba 26, 2025.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...