Mkuranga, 24 Oktoba 2025 —

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mkuranga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Abdallah Ulega, amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuendelea kuiamini na kuichagua CCM katika uchaguzi mkuu ujao ili kuimarisha maendeleo yaliyokwisha kuanza chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ulega ameyasema hayo leo wakati akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kijiji cha Kisiju Pwani, Kata ya Kisiju, wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani.

Akizungumza wananchi, Ulega amesema maendeleo yanayoonekana leo Mkuranga na maeneo mengine ya Mkoa wa Pwani ni matokeo ya uongozi imara wa CCM na Dkt. Samia, ambaye ameweka kipaumbele katika kuboresha miundombinu, huduma za jamii na kuinua kipato cha wananchi.

“Wananchi wenzangu wa Mkuranga, ninawaomba tuendelee kuiamini CCM. Chama chetu ndicho kinachotekeleza ahadi. Mama yetu Dkt. Samia amefanya mambo makubwa—kutoka kwenye ujenzi wa barabara, bandari, shule, na miradi ya maji—na sasa ni zamu yetu kuhakikisha tunaendeleza haya kwa kumpa kura yeye na wagombea wote wa CCM,” alisema Ulega.

Ameongeza kuwa wananchi wa Kisiju hawapaswi kusahau ahadi za Dkt. Samia ambazo tayari zimeanza kutekelezwa, ikiwemo boti alizozileta kwa ajili ya kusaidia shughuli za usafiri na uvuvi katika maeneo ya mwambao.

“Boti alizozileta Dkt. Samia ni mali ya wananchi wa Kisiju. Zimeletwa kwa ajili ya kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku—uvuvi, biashara, na huduma za kijamii. Hivyo tunapaswa kulinda mali hizi na kuendelea kuunga mkono serikali yetu,” alisisitiza Ulega.
Katika hotuba yake, Ulega pia alitoa ahadi mpya za kimaendeleo, akibainisha kuwa serikali ya CCM itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo.

“Ninawaahidi ndugu zangu, tutajenga vivuko kwaajili ya wananchi wanaoshi kwemye visiwa mbalimbali kuja Kisiju Pwani, na kutoka Kisiju kuunganisha visiwa hivyo ili kurahisisha usafiri. Pia tutajenga madarasa mapya katika shule za msingi na sekondari katika vijiji vya Kisiju na Kelekese. Ni wakati wa Kelekese kunufaika na miradi ya maendeleo kama ilivyokuwa kwa vijiji vingine,” alisema.

Aidha, Ulega alimshukuru Rais Samia kwa ujenzi wa Bandari ya Kisiju, akisema mradi huo utakuwa mkombozi mkubwa wa kiuchumi kwa wananchi wa Mkuranga.

“Tunamshukuru sana Mama yetu Dkt. Samia kwa kutuaidi kujenga Bandari ya Kisiju. Hii ni bandari ya kimkakati itakayoongeza ajira, kukuza biashara za uvuvi na utalii, na kuinua uchumi wa wananchi wetu wa Pwani,” alisema Ulega kwa msisitizo.
Kwa upande wake, Meneja wa Kampeni za CCM Jimbo la Mkuranga, Bw. Juma Abeid, aliwataka wananchi wa Kisiju na maeneo jirani kuhakikisha wanawachagua wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi ya Rais, Mbunge, hadi Madiwani.
“Wananchi wa Mkuranga, tusirudishe nyuma maendeleo tuliyoanza kuona. Ili ahadi hizi zote zitimie, ni lazima tumchague Rais wetu Dkt. Samia, tumchague Mheshimiwa Ulega, na madiwani wetu wote wa CCM. Chama chetu hakiahidi maneno—kinatekeleza kwa vitendo,” alisema Abeid.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa CCM ngazi ya wilaya, wazee wa chama, vijana, na wanawake, ambapo wananchi wengi walionyesha hamasa kubwa ya kuunga mkono chama hicho tawala katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

















 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...