Kibaha, Pwani
TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imesisitiza umuhimu wa wabunifu kulinda bunifu zao kabla ya kuziingiza sokoni, kwa lengo la kulinda haki zao, kuongeza thamani ya bunifu hizo na kuhakikisha zinachangia maendeleo ya kiuchumi nchini.

Kauli hiyo imetolewa jana Oktoba 17,2025 na Dkt. Erasto Mlyuka, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uendelezaji na Uhawilishaji Teknolojia (CDTT), akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya siku tano kwa wabunifu wa teknolojia za kilimo na mifumo ya chakula nchini.

Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) mkoani Pwani, na yamefadhiliwa na Shirika la Chakula Duniani (WFP) kama sehemu ya juhudi za kuendeleza bunifu zinazoweza kuimarisha uzalishaji na usalama wa chakula.

Katika hotuba yake, Dkt. Mlyuka alisema kuwa ulinzi wa bunifu ni msingi muhimu wa mafanikio ya wabunifu, hasa katika mazingira ambayo teknolojia na maarifa ni nyenzo kuu za maendeleo.

“Mafanikio ya bunifu yoyote hayawezi kupatikana kwa juhudi binafsi pekee. Tunahitaji mifumo ya pamoja inayowawezesha wabunifu kushirikiana, kulindwa na kunufaika kiuchumi kutokana na kazi zao,” alisema Dkt. Mlyuka.

Kwa upande wake, Bw. Benedickson Wilson Byamanyilwowa, Afisa Usajili kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), alisema kwa siku tano mfululizo wamekuwa wakitoa elimu juu ya miliki bunifu kwa wabunifu mbalimbali wa teknolojia za chakula na nyenzo zenye uwezo wa kuzalisha chakula nchini.

“Hii inatokana na malengo ya dunia ya kuhakikisha tunaondokana na changamoto ya upungufu wa chakula. Tutaendelea kutoa elimu na kuhakikisha wabunifu wanapata hati halali za ulinzi wa bunifu zao,” alieleza Byamanyilwowa.
Miongoni mwa wabunifu walioshiriki ni Bw. Akram Ali Omari, mbunifu wa mfumo wa “Fugaj Smart” kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA). Mfumo huo unalenga kurahisisha shughuli za ufugaji kwa kutumia teknolojia ya sensa na ukusanyaji wa taarifa kwa njia ya kidijitali.

Pia, Dkt. Whitefrank Frank, mbunifu kutoka kampuni ya AFRIMIX ANIMAL FEEDS, aliwasilisha bunifu ya chakula cha kuku aina ya Broila, kinachoongeza uzito wa kuku kwa muda mfupi bila kuathiri ubora wa nyama.

Wabunifu hao wamesema bunifu za kilimo zikitumika ipasavyo zinaweza kuchochea mapinduzi ya kilimo nchini, kuongeza tija kwa wakulima na wafugaji, na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Mafunzo hayo yalitolewa na wataalamu kutoka COSTECH, BRELA, na Kituo cha Ubunifu wa Teknolojia Dar es Salaam (DTBi), ambapo jumla ya wabunifu 10 walishiriki. Washiriki walipata maarifa kuhusu usajili wa bunifu, haki miliki, na mbinu za kuziendeleza kuwa bidhaa au huduma za kibiashara.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...