Saidi Mwishehe,Michuzi TV-Butiama

MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM)Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema Chama hicho kinatambua umuhimu wa kuimarisha zaidi mshikamano wa Watanzania kwa kukamilisha mchakato wa Katiba mpya kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi Mkuu 2025-2030.

Akizungumza leo mbele ya wananchi wa Wilaya ya Butiama mkoani Mara ambako ameendelea na mikutano ya kampeni kuomba kura kuelekea Oktoba 29 mwaka huu, Dk.Samia ametumia nafasi hiyo kuelezea mchango wa Baba wa Taifa Mwalimu Julisu Nyerere sambamba na kuelezea miradi iliyokuwa ndogo za Nyerere kwa Watanzania.

Kuhusu Katiba Mpya amesisitiza Chama Chq Mapinduzi (CCM)kinatambua umuhimu wa kuimarisha zaidi mshikamano wa Watanzania kwa kukamilisha mchakato wa Katiba mpya kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi Mkuu.

"Haya ni matakwa ya makundi mbalimbali ya Watanzania kwa nyakati tofauti. Tulijaribu wakati wa awamu ya nne mchakato haukukamilika, awamu ya sita tunakwenda kuendeleza mchakato huo.

"Kama walivyofanya waasisi wa taifa na chama chetu, nasi tutaendelea kulinda chama cha mapinduzi katika kusimamia yote hayo kwa maslahi mapana ya Watanzania kwani Baba wa Taifa letu alisema bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba," amesema na kusisitiza hatakubali nchi yetu iyumbe kwa kisingizio chochote kile.

Akimueleza zaidi Mwalimu Nyerere Mgombea Urais Dk.Samia amesema Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ni vigumu kumtenganisha na misingi ya falsafa aliyoijenga nchini ikibebwa na dhana ya uhuru na umoja, uhuru na kujitegemea, uhuru na kazi, uhuru na wajibu na dhana zingine muhimu za kiitikadi.

Dk.Samia amesema kwamba dhana hizo alizianzisha kwa lengo la kuleta umoja na mshikamano nchini kwa lengo la kujenga taifa imara lenye kutegemea na kujali maendeleo ya watu.

"Alisisitiza kuwa maendeleo yote yenye maana hayana budi kuwalenga watu ndiyo maana dira na mipango yetu ya maendeleo pamoja na ilani za Chama Cha Mapinduzi zinajielekeza kujenga taifa linalojitegemea lenye uchumi jumuishi na ustawi wa watu.

"Yaani maendeleo ya jamii, uwezeshaji wa kiuchumi na kukuza uchumi mkubwa wa taifa letu," amesema Dk.Samia amesema Serikali imeweza kutekeleza miradi mikubwa ya utawala bora inayotoa msukumo kwenye sekta za uzalishaji ambayo ni sehemu ya ndoto ya Mwalimu Nyerere.

Ameitaja miradi hiyo ni utekelezaji mpango wa kuhamisha makao makuu ya nchi Dodoma."Tuliamua miaka ile kwamba makao makuu ya nchi yetu yatakuwa Dodoma, tumechelewa kidogo lakini kuanzia awamu ya tano na hii ya sita tumekamilisha uhamiaji wa serikali na kuifanya makao makuu iwe Dodoma.

Aliongeza: "Mihimili yote mitatu ya serikali tayari ipo Dodoma, Bunge lilitangulia, serikali tukafuata na Mahakama mwaka 2024 imehamia Dodoma."

Mgombea Urais Dk.Samia amesema jambo lingine ambalo lilikuwa ndoto ya Mwalimu Nyerere ni ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Julius Nyerere.

Amefafanua kwamba bwawa hilo alitaka lijengwe kipindi chake lakini hali haikuruhusu hata hivyo kwa sasa serikali imeshakamilisha ujenzi wa bwawa hilo.

“Mradi mwingine alioutaja ni mradi wa maji Same - Mwanga ambako alijenga bwawa la Nyumba ya Mungu lakini hakuweza kuuendeleza mradi huo.”

Amesema serikali imeundeleza na kuukamilisha mradi huo ambapo sasa wananchi wa Same, Mwanga na Korogwe wanafaidika na mradi huo.

Aliyataja mabwawa mengine ambayo Hayati Mwalimu Nyerere alitaka yajengwe ni bwawa la Mkomazi lililopo Korogwe ambalo limefikia asilimia 50 na bwawa la Kidunda ambalo lingesaidia maji kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Pwani na sehemu ya Morogoro.

Ameongeza bwawa hilo ujenzi wake upo asilimia 50."Zile ndoto za Mwalimu za utawala bora, sekta za uwezeshaji wananchi kiuchumi, maendeleo ya jamii ndiyo haya ambayo tunaendelea kutekeleza.

"Baba wa Taifa alituachia misingi mizuri kifalsafa, kisera na kisiasa. Kazi yetu ni kutafsiri misingi ile na fikra zile katika mazingira ya sasa," amesema na kuongeza Serikali itaendelea kudumisha tunu za amani, umoja, mshikamano wa taifa na muungano.


















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...