Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Mara

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Steven Wasira, amewataka wananchi kuchukua tahadhali dhidi ya kikundi cha watu wachache ambao wanaoleta chokochoko katika mitandao ya kijamii.

Wasira ameyasema hayo leo Oktoba 9,2025 alipokuwa katika mkutano wa kampeni za mgombea Urais kupitia Chama Cha Mqpinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye ameanza kampeni katika Mkoa wa Mara akitokea mkoani Mwanza.

Amesema kuwa kikundi hicho ni miongoni mwa wachache wasioridhika hata hivyo kamwe hawatoweza kutimiza dhamira yao ovu huku akifafanua amani na utulivu itaendelea kutawala nchini.

Wasira aliyekuwa akizungumza mbele ya Dk.Samia katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya Wana Bunda amesema kuwa zipo chokochoko za watu wacheche wanaotumia mitandao ya kijamii. “Naomba msome ile mitandao kwa makini sana. Kuna watu watu hawaridhiki.”

Wasira amesema “Kinamama wanaopika maharage wanafahamu yapo maharage hata ukiyapika vipi yatatokea machache yakielea. Hayo hayaivi na ndiyo watu wanaosumbua.”

“Watu hao hawawezi kuisumbua nchi, namwambia mgombea wetu (Dk. Samia) asibabaishwe na watu hao wachache, hata ukifanya vizuri namna gani wao wananuna, ndivyo walivyo."

"Wapo watakaokumbuka kwa wema wenye nia njema. Dk. Samia amefanyakazi kubwa, jinsi mnavyomuunga mkono hapa ndivyo anavyoungwa mkono Tanzania nzima," amesema Wasira.

Ameongeza kuwa CCM imewaletea mgombea Urais mwenye mafanikio makubwa ya utekelezaji Ilani ya uchaguzi iliyopita na siyo mwenye uwezo mdogo.

"Hatuwaletei mgombea Urais 'lena' tunawaletea mgombea Urais aliyefanyakazi ya Urais kwa mafanikio makubwa," amesisitiza

Akieleza zaidi Wasira amesema Dk. Samia aliingia madarakani katika misukosuko wakati ambao taifa lilikumbwa na ugonjwa wa Uviko 19, kufariki kwa Rais aliyekuwa madarakani (Hayati Dk. John Magufuli) na kushuka kwa uchumi.

Amesema Dk. Samia alipoingia madarakani alitumia maneno mawili ambayo ni 'Kazi Iendelee'.

"Alipewa mtihani mkubwa aliachiwa miradi mikubwa ya nchi yetu. Aliachiwa reli haijakamilika lakini leo imekamilika mpaka Makutupora ya Singida kilometa 722 kutoka Dar es Salaam.

"Aliachiwa bwawa la Mwalimu Nyerere lilikuwa chini ya asilmia 30 hata hivyo asilimia 70 imejengwa chini ya usimamizi wa Rais Samia na Tanzania ina umeme wa kutosha.”

Kwa upande wa elimu, Wasira amesema katika Wilaya ya Bunda Dk. Samia amejenga shule mpya 13 za msingi, shule 15 za sekondari, zahanati 20, vituo vitatu vya afya na hospitali moja mpya.

Pia ametoa mchango mkubwa kupunguza vifo vya kinamama na watoto kwani ulipoingia madarakani alikuta katika kila vizazi hai 100,000 vizazi 500 walifariki dunia kila mwaka.

“Dk. Samia amewezesha kushusha hali hiyo ambapo sasa katika kila vizazi hai 100,000 mia tano walikuwa wakifarkki leo vimeshuka kufikia 100.

Awali, Mgombea Ubunge Jimbo la Pangani, Jumaa Aweso, alisema alipokabidhiwa Wizara ya Maji, alipewa maagizo na Dk. Samia kuhakikisha hakuna mwanamke atakayeteseka kwa kukosa maji.

Amesema hali ya maji miaka minne iliyopita katika wilaya hiyo ilikuwa mbaya kwani miradi iligeuka kichaka cha watu kufanya ubadhirifu.

Amefafanua Dk. Samia alimuagiza kufika wilayani Bunda kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo huku akitoa fedha sh. bilioni 10 kutekeleza mradi wa maji Nyabeho.

"Hapa tuna miradi mingi ambayo ipo ilikamilika na mengine ipo hatua mbalimbali kwa gharama ya sh. bilioni 20. Zaidi ya wananchi asilimia 87 eneo la Bunda Mjini wanapata huduma ya maji," alieleza.

“Maeneo yaliyokuwa na changamoto ya maji ni vijijini ambapo Dk. Samia amechukua hatua kuhakikisha huduma hiyo inapatikana,”amesema na kuongeza Dk.Samia ametoa fedha zaidi ya sh. bilioni 100 kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Bunda na Tarime




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...