.jpeg)
Na Karama Kenyunko,Michuzi TV
KAMPUNI ya bima ya Jubilee Insurance imeamua kushirikiana na Chama cha Waendesha Baiskeli Tanzania katika kudhamini safari ya wanachama wanne wa chama hicho kushiriki mashindano makubwa ya kimataifa ya Live Free Race 2025, yatakayofanyika jijini Nairobi, Kenya kuanzia Oktoba 5 mwaka huu.
Akizungumza leo Oktoba3,2025 wakati wa kutambulisha udhamini wa wanamichezo hao jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Jubilee Holdings, Dkt. Harlod Adamson, amesema udhamini huo unaakisi dhamira ya kampuni hiyo katika kukuza michezo na kuimarisha afya kwa Watanzania, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Michezo ni afya na pia ni ajira. Kupitia udhamini huu tunataka kuona vijana wetu wanatimiza ndoto zao, wakipeperusha bendera ya taifa na kuwa mfano wa nidhamu, mshikamano na bidii. Jubilee imekuwa ikifadhili mashindano haya kwa miaka kadhaa sasa, na mwaka huu tumeona umuhimu wa kushirikiana na Chama cha Waendesha Baiskeli Tanzania ili kuwapa nafasi vijana wetu kuonyesha uwezo wao,” amesema Dkt. Adamson.
.jpeg)
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Fedha wa Jubilee Life Insurance, Bw. Hilary Godson, aliyemuwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu, Bi. Hellen Mzena, amesema udhamini huo si msaada pekee bali ni dhamira ya dhati ya kampuni hiyo kusimama na vijana na jamii kwa ujumla.
“Kwa Jubilee, huu ni uwekezaji katika afya, vipaji na mustakabali wa vijana. Tunafadhili usafiri, gharama za ushiriki, tiketi za kuingia, chakula, malazi, bima ya afya na fedha za kujikimu. Tunaamini kupitia nafasi hii, vijana wataishi maisha yenye furaha, bila msongo, na kufanikisha ndoto zao,” amesema Bw. Godson.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kukuza Vipaji wa Chama cha Baiskeli Tanzania, Dkt. Judith Mashala, ameishukuru Jubilee Insurance kwa udhamini huo na kueleza kuwa vijana hao wanne wamepata nafasi ya kushiriki mashindano makubwa yanayojulikana pia kama Gran Nairobi, yakihusisha mataifa mbalimbali ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania, yakiwa na washiriki zaidi ya 3,000.
“Timu yetu ilitoka kushiriki mashindano makubwa nchini Rwanda wiki mbili zilizopita na sasa kupitia Jubilee, vijana wanne wameungana na wenzao Nairobi. Tunaamini wamejiandaa vizuri na watafanya vyema kupeperusha bendera ya Taifa. Tunaomba Jubilee iendelee kushirikiana nasi kwani mchezo wa baiskeli ni fursa muhimu kwa vijana na taifa letu,” amesema Dkt. Mashala.
Mashindano hayo ya kimataifa yanayoandaliwa kila mwaka na Jubilee Holdings, yameendelea kuwa kivutio kikubwa cha michezo Afrika Mashariki, yakishirikisha wanariadha chipukizi na mabingwa waliowahi kutamba kwenye michezo ya baiskeli duniani.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...