SERIKALI imetambua sekta ya kahawa kama nguzo muhimu ya uchumi wa kilimo nchini, kutokana na mchango wake mkubwa katika kuongeza ajira, kipato cha wananchi na mapato ya taifa, hasa kwa zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanaojihusisha moja kwa moja na shughuli za kilimo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa msimu wa sita wa Tamasha la Kahawa (Kahawa Festival) linalofanyika kwa siku tatu katika kiwanda cha Coffee Curing mjini Moshi, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Benson Ndiege, alisema sekta ya kahawa na ushirika ni mfano halisi wa ushirikiano unaoleta matokeo chanya ya kiuchumi kwa jamii.
“Ushirika na Bodi ya Kahawa ni mfano wa umoja unaoshirikiana kufanya kazi kwa pamoja. Serikali inatambua umuhimu wa zao hili kwa sababu zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo, na sehemu kubwa yao wanaguswa na kahawa,” alisema Dkt. Ndiege.
Alibainisha kuwa serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kuinua zao la kahawa kupitia utoaji wa miche bure milioni 20, ruzuku za pembejeo na mikakati ya kuongeza tija kwa wakulima wadogo, hatua inayolenga kufufua ari ya uzalishaji katika mikoa ya kanda ya kaskazini na maeneo mengine ya kimkakati.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kahawa Festival,Dennis MAulu alisema tamasha la mwaka huu limejikita katika uhamasishaji wa kahawa, likilenga kutambua mchango wa wakulima katika tasnia hiyo, kukuza biashara za ndani na nje, pamoja na kuelimisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya kahawa na mbolea.
“Maonyesho haya ni mwendelezo wa Siku ya Kahawa Duniani. Sisi kama Kaskazini tukaona siku moja haitoshi, tukaongeza hadi siku tatu ili wadau waweze kupata fursa ya kutosha kufanya yale ambayo yanaongeza biashara zao na tasnia ya kahawa,” alisema Prof. Kamuzoram.
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Primus Kimaryo, alisema ipo haja ya kujenga uelewa wa pamoja kuhusu kahawa ya Tanzania ili kuondoa sintofahamu inayojitokeza kati ya wazalishaji na watumiaji wa mwisho wa bidhaa hiyo.
“Nchi yetu inapokea wageni mbalimbali. Akiingia hotelini anaambiwa Tanzania inalimwa kahawa, akienda kwenye maduka makubwa anaambiwa Tanzania inalimwa kahawa, akienda migahawani anaambiwa Tanzania inalimwa kahawa — lakini wakinywa, panatokea sintofahamu,” alisema Kimaryo.
Tamasha la Kahawa 2025 limekusanya wadau zaidi ya 50 kutoka sekta mbalimbali, likiwa ni sehemu ya kampeni endelevu ya kukuza biashara ya kahawa, kuongeza ubora wa bidhaa, na kuhamasisha unywaji wa kahawa ya ndani kama sehemu ya utamaduni wa Watanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...