Na Mwandishi Wetu, Lindi
VIONGOZI wa dini mbalimbali kutoka mikoa ya Kanda ya Kusini wamewataka vijana nchini kuendelea kulinda amani ya Taifa, kuacha kutegemea taarifa za mitandaoni na badala yake kujitokeza kwa wingi kupiga kura kumchagua kiongozi wanayemtaka katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Wito huo umetolewa leo Oktoba 24, 2025, katika Kongamano la Amani lililofanyika mkoani Lindi, likijumuisha viongozi wa dini kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Katika kongamano hilo, viongozi hao walijadili mada mbalimbali kuhusu umuhimu wa kupiga kura, historia ya chaguzi nchini na wajibu wa kila raia kulingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza katika kongamano hilo, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Sheikh Jamaldin Chamwi, amewataka wananchi kutumia haki yao ya kupiga kura kwa amani na utulivu, akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi ya umoja na upendo.

“Kwa yale tunayoyaona mitandaoni, tuwaambie wanaotaka vurugu kwamba Tanzania siyo kama wanavyofikiria. Njia bora ya kuonesha msimamo wetu ni kujitokeza kwa wingi kupiga kura,” amesema Sheikh Chamwi.

Naye Mwakilishi wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Padri Bonavomtura Makota, amesema wanaamini katika nguvu ya vijana na kuwaasa kupokea kile wanachoshauriwa na wazee ili kudumisha amani.

Kwa upande wake kiongozi mwandamizi wa Kamati ya Amani Mkoa wa Ruvuma, Elimu Mwenzegule amesema kuwa wanaunga mkono jitihada za kuhakikisha amani inakuwepo nchini.

Mwenyekiti wa Makanisa Wilaya ya Nachingwea, Mchungaji Leonard John amesema katika historia ya nchi kwa chaguzi zote zilizopita haijawahi kutokea uvunjaji wa amani hivyo kuwaasa viongozi wenzake wa dini kuendelea kufanya jukumu lao la kuhubiri amani.

Abdallah Mpenda ambaye ni Mwenyekiti wa vijana Baraza Kuu ya Waislamu wa Tanzania (BAKWATA), Mkoa wa Ruvuma, amesema vijana wanatakiwa kutafakari mambo kabla kuchukua uamuzi ili kuepuka kujazwa chuki na hasira.

“Tusiwe wenye kufanya maamuzi kwa masikio bali kwa tufanye kwa kuona kwa macho yetu, tuangalie hali tuliyokuwa nayo kwenye nchi yetu tunaiona namna gani na kuangalia wale ambao sehemu zao wamekosa amani, wamekosa utulivu, wamekuwa na vurugu, wapo katika hali gani. Halafu tuangalie je tunaweza kumudu yale wanayopitia wenzetu?,” ameeleza Mpenda.

Akichagia mada Mchungaji Lussie Ngongi, amesema ni muhimu viongozi wa dini kuhubiri amani, haki, uhuru kwa watu na kusisitiza kujitokeza kupiga kura Oktoba 29, 2025.

“Hatuna nchi nyingine zaidi ya Tanzania, tukumbuke kuilinda Amani ya Taifa letu,” amesema.

Katibu wa Jumuiya ya Vijana Mkoa wa Mtwara, Mussa Khamis amesisitiza kuwa amani ni jambo la msingi kwa ustawi wa kuendesha maisha ya kila siku na kiibada.

“Ili tupate amani lazima tujitokeze siku ya tarehe 29 kupiga kura, kuchagua viongozi ambao tutasaidiana nao katika nchi hii kulinda amani na kuziba upenyo wowote unaoashiria kuvunja amani ya nchi hii,” amesistiza.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...