Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesema uanzishwaji wa Chuo cha Ufundi Dodoma (DTC) ni hatua kubwa ya Serikali katika kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023 pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza Novemba 27, 2025, Naibu Waziri amebainisha kuwa chuo hicho kimekusudiwa kuwa kitovu cha utoaji wa elimu ya ufundi bora nchini, kitakachowawezesha vijana kupata ujuzi na stadi za kazi zitakazowaandaa kushiriki kikamilifu katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.
Aidha, amesisitiza kuwa lengo kuu la Serikali ni kuhakikisha taifa linakuwa na nguvu kazi yenye ujuzi, ubunifu na ushindani wa kimataifa.
Naye Naibu Katibu, Dkt. Hussein Mohamed Omar, amesema awamu ya kwanza ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Dodoma imehusisha ujenzi wa madarasa, mabweni, ofisi, karakana pamoja na ununuzi wa samani zote muhimu ili kuhakikisha mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia.
Aidha, Dkt. Omar amesisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendeleza ujuzi nchini na kuwa Wizara itaendelea kukisaidia chuo hicho ili kiweze kujiendesha kwa ufanisi na kutoa mafunzo ya ufundi stadi yatakayowawezesha wanachuo kupata ujuzi wa vitendo, kujiajiri na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Prof. Preksedis M. Ndomba, amesema tayari watumishi saba wameajiriwa kwa ajili ya kuendesha shughuli za Dodoma Technical College (DTC), huku maandalizi yakiendelea kuhamisha baadhi ya watumishi kutoka DIT.
Ameongeza kuwa mahitaji ya kada 39 mpya yameshaainishwa na kuwasilishwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Prof. Ndomba ameeleza kuwa ujenzi wa miundombinu ya maji safi, maji taka na barabara umefikia asilimia 15, sambamba na usimamizi wa mikataba ya samani na vifaa vya zimamoto.
Aidha, DTC imeomba kusajiliwa na kutambuliwa na NACTVET, na mara miundombinu itakapokamilika, ambapo ukaguzi wa mwisho utafanyika ili kukamilisha hatua za usajili wa chuo hicho.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...