Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Kituo cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali na Taarifa (MECIRA), Habibu Mchange, amesema ndani ya siku 24 tu tangu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan aanze muhula wake wa pili wa uongozi, tayari kuna dalili wazi za kasi mpya, busara ya kiutawala na mabadiliko makubwa katika sekta muhimu za nchi.

Amesema tathmini ya awali inaonyesha kuwa maelekezo ya Rais Samia kwa mawaziri, makatibu wakuu, taasisi na wasimamizi wa miradi yameanza kutafsiriwa kwa vitendo, hali inayoleta matumaini mapya kwa wananchi.

Nishati: Miradi Yakamilishwa, Urasimu Watoweka
Mchange amesema sekta ya nishati imeendelea kuonyesha uhai mpya kupitia kukamilika kwa JNHPP na miradi mingine ya kuongeza uzalishaji wa umeme, sambamba na agizo la TANESCO kuongeza kasi ya kuwaunganisha wananchi na wawekezaji bila urasimu.

Amesema msisitizo wa kuwekeza kwenye nishati jadidifu kama upepo, solar na gesi unaipa Tanzania msingi mpya wa uchumi wa kisasa na unaofungua ajira nyingi kwa vijana.

Miundombinu: Ufuatiliaji Mkali na Ujenzi kwa Viwango
Katika sekta ya miundombinu, Mchange amesema serikali imeanza kusukuma kukamilika kwa barabara, madaraja, viwanja vya ndege, bandari na vivuko ambavyo vilikuwa vimesimama kwa muda mrefu.

Amesema hatua hizo zinatuma ujumbe wa uongozi wa matendo unaofungua maeneo mapya ya uwekezaji na biashara.

Afya: Huduma Kuanza Mara Moja, Utu Kuwekwa Mbele

Akichambua sekta ya afya, Mchange amesema Rais Samia ameonyesha kipaumbele cha kipekee kwenye huduma za watu kupitia maagizo ya kuanza huduma katika hospitali na vituo vilivyokamilika, kuhakikisha dawa zinapatikana, kutotoa vikwazo kwa wajawazito na kuruhusu miili iliyokuwa ikizuiliwa kutokana na kushindwa kulipia.

Amesema hatua hizo zinathibitisha serikali inayoweka utu na uhai mbele ya taratibu.

Maji: Kasi ya Utekelezaji Yakomaa
Kwa mujibu wa Mchange, sekta ya maji imepewa kipaumbele kwa maagizo ya kukamilisha miradi iliyokwama, kupunguza upotevu wa maji kwa teknolojia na kusukuma utekelezaji katika maeneo yenye ukame na changamoto za muda mrefu.

Sheria: Busara, Maridhiano na Kurejesha Amani
Akitaja tukio la Oktoba 29, Mchange amesema uamuzi wa kusimamia mchakato uliowezesha kuachiwa kwa vijana waliokamatwa ni “ishara ya uongozi wenye busara, maridhiano na nia ya kuponya taifa.”

Amesema hatua hiyo inaonyesha serikali inayosikiliza wananchi, wazazi na viongozi wa dini, huku ikiweka mbele maslahi mapana ya taifa.

Ameongeza kuwa kuna mwanga wa mageuzi katika uhuru wa mahakama, uwajibikaji wa vyombo vya uchunguzi na mwelekeo wa kuondoa sheria kandamizi.

Kilimo: Msingi Mpya wa Uchumi wa Vijana
Mchange amesema hatua za kupunguza bei ya mbolea, kuongeza skimu za umwagiliaji na kupanua viwanda vya usindikaji zinakuza kasi ya sekta ya kilimo na kuifanya kuwa nguzo muhimu kwa vijana na wakulima wadogo.

Mifugo: Ufugaji wa Kisasa Wapewa Nguvu
Amesema serikali imeongeza upatikanaji wa chanjo, kusukuma ujenzi wa minada ya kisasa, viwanda vya nyama na maziwa, hatua zinazokuza uchumi wa ufugaji na uwekezaji katika ranchi na malisho.

“Tanzania Ipo Kwenye Historia Mpya” – Mchange
Akimulika mwelekeo wa siku 24 za mwanzo, Mchange amesema kuna dalili zote za uongozi wenye uthabiti, kasi, nidhamu na ujasiri wa kufanya maamuzi magumu kwa maslahi ya wananchi.

Amesema ikiwa mwanga huu utaendelea, Tanzania itaingia katika “historia mpya ya umoja, amani, fursa na maendeleo kwa wote.”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...