Na. Philipo Hassan - Mikumi.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) leo Novemba 25, 2025 ameielekeza TANAPA kuhakikisha inafanya kazi kwa kuzingatia utu ili kuboresha ustawi wa jamii. Dkt. Kijaji aliyasema hayo katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Mikumi.
“Tuendeleeni kuzingatia kaulimbiu ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani katika kutoa huduma zetu za uhifadhi na utalii kwa kuweka utu mbele ili kuimarisha ustawi wa watanzania” alisema Dkt. Kijaji
Pamoja na hayo Dkt. Kijaji alisisitiza kuwa wabunifu katika kutangaza vuvutio vya utalii vinavyopatikana katika Hifadhi za Taifa Tanzania ili kufikia adhma na malengo ya Serikali ya kufikisha watalii milioni 8 ifikapo mwaka 2030.
Naye, Mhe. Adam Malima, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro aliipongeza TANAPA kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uzalendo mkubwa hivyo kuifanya Morogoro kuendelea kunga’aa kupitia sekta ya uhifadhi na utalii.
“Lengo la Mkoa wa Morogoro ni kuwa kitovu cha utalii nchini Tanzania kwa kuwa tuna jumla ya hifadhi za Taifa tatu Hifadhi ya Taifa Mikumi, Milima ya Udzungwa na Nyerere. Hivyo ni jukumu letu kushirikiana na TANAPA katika kuhakikisha tunakuza uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Morogoro kupitia sekta ya uhifadhi na utalii” alieleza Mhe. Malima.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi TANAPA Musa Nassoro Kuji alieleza kuhusu maendeleo ya miundombinu katika hifadhi, ongezeko la mapato na watalii katika hifadhi hiyo.
“Kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26, hifadhi imetembelewa na jumla ya watalii 62,468, sawa na ongezeko la asilimia 1.18% ukilinganisha na matarajio ambayo yalikuwa kufikisha watalii 61,742. Pia kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026, hifadhi imekusanya jumla ya kiasi cha Tsh. bilioni 3.9 sawa na ongezeko la 15.44% ya matarajio alisema Kamishna Kuji.
Aidha, ziara ya Mhe. Dkt. Kijaji ilihusisha ukaguzi wa miradi inayotekelezwa Hifadhi ya Taifa Mikumi ambayo ni pamoja na lango la kuingilia watalii la Doma, kituo cha kutolea taarifa kwa wageni (VIC), mradi wa eneo la kupumzikia wageni na kula chakula (Picnic Site), mradi wa uwanja wa ndege, mradi wa kambi ya kulala watalii na mradi wa nyumba za kulala watalii (Bandas).
Ziara hiyo iliambatana na viongozi mbalimbali wa Wizara ikiwa ni pamoja na Mhe. Hamad Chande (Mb) Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Thereza Mugobi Mkurugenzi wa Idara ya Utalii.














Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...