Na Saidi Lufune, Iringa
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha miundombinu katika hifadhi za taifa na vivutio vya utalii nchini, hatua inayolenga kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi.
Waziri Dkt. Kijaji ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha.
Amesema kuwa ili kufikia lengo la kuvutia watalii milioni nane, Wizara itaendelea kushirikiana na wadau katika kutangaza na kuuza bidhaa mbalimbali za utalii zilizopo nchini.
Aidha, ameeleza kuwa zaidi ya sh.bilioni 58 zimetumika kuwekeza katika ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege, pamoja na majengo mbalimbali ya malazi kwa ajili ya wageni na watumishi ndani ya hifadhi hiyo.
Dkt. Kijaji ameuagiza uongozi wa Hifadhi ya Taifa Ruaha kufanya kazi kwa ukaribu na viongozi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo, ili kubaini maeneo yanayoweza kuingizwa katika mpango wa ushirikiano na wawekezaji kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kisasa ili kuendana na maboresho makubwa yaliyofanyika ndani ya hifadhi hiyo kupitia Mradi wa REGROW.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Hassan Chande, amepongeza uongozi wa TANAPA kwa kusimamia vyema utekelezaji wa miradi hiyo, akisema kuwa itaongeza mahusiano mazuri kati ya wahifadhi na wananchi, pamoja na kuchochea ajira na kuongeza kipato kwa jamii zinazozunguka hifadhi.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Diwani wa Kata ya Idodi, Mhe. Julius Mguta, ameishukuru Serikali kwa kuendeleza miundombinu iliyoachwa na uliokuwa Mradi wa REGROW na kwamba imesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha maendeleo ya wananchi wa kata hiyo kwa kuwaongezea kipato cha kila siku na kuwafanya kuachana na shughuli haramu ikiwemo ujangili.



.jpeg)

.jpeg)



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...