UZINDUZI wa kitabu Tawasifu ya Mhe. Balozi Daniel Ole Njoolay umefanyika jijini Arusha kwa shamrashamra, ukihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwamo Mgeni Rasmi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA Amos Makalla, wabunge, viongozi wa chama na wadau wa tasnia ya uchapishaji.
Katika hafla hiyo, Prof. Raymond S. Mosha, aliyeteuliwa na kamati ya maandalizi kutoa muhtasari wa yaliyomo kwenye kitabu hicho, aliwasisimua wageni kwa maelezo yake akieleza namna kitabu hicho kinavyomnasa msomaji kutokana na uwezo wa kipekee wa Balozi Njoolay katika kusimulia simulizi za maisha. Alisema kitabu hicho ni zaidi ya tawasifu ya kawaida, bali ni hazina ya mafunzo, busara na safari ndefu ya uongozi, maadili, uaminifu na utumishi kwa taifa.
Prof. Mosha alinukuu maneno ya viongozi wakuu wastaafu waliolipatia kitabu hicho heshima ya kipekee, akiwamo Waziri Mkuu Mstaafu Joseph Sinde Warioba, aliyeandika Dibaji, pamoja na hayati Rais Benjamin Mkapa ambaye alimpongeza Balozi Njoolay kwa uthubutu wa kusema ukweli bila kujali unamkera nani.
Akizungumzia kina cha kitabu hicho, Prof. Mosha alisema mashiko ya simulizi za Balozi Njoolay yanamfanya afanane na wazee wa kale waliokuwa mabingwa wa hadithi, na kuongeza kuwa kazi hiyo inapaswa kutafsiriwa kwa Kiingereza ili dunia iweze kujifunza safari yake. Alisisitiza kuwa kitabu hicho ni ushahidi hai wa namna mwandishi alivyojibu wito wa kulitumikia taifa kwa moyo mkunjufu na kwa maadili ya hali ya juu.
Hafla hiyo ilimalizika kwa wito wa viongozi na wadau kuendelea kumtumia Balozi Njoolay katika majukumu muhimu ya nchi, wakimtambua kama hazina isiyopimika kwa Taifa la Tanzania.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...