Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Mkuu wa Harvard Kennedy School, Prof. Jeremy M. Weinstein baada ya mazungumzo yao huko Marekani)

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeingia katika mazungumzo ya ushirikiano wa kimkakati na Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani, yakilenga kuimarisha matumizi ya Akili Mnemba (AI) katika elimu, utafiti na uchambuzi wa taarifa.

Mazungumzo hayo yalianzishwa na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, alipokuwa katika ziara ya kikazi nchini Marekani.

Ushirikiano huo unalenga kujenga uwezo wa kutumia AI kwa ufanisi katika kufundishia, kuongeza kasi ya tafiti, na kurahisisha uchakataji wa taarifa nyingi kwa wakati mfupi, eneo ambalo linazidi kuwa muhimu katika vyuo vikuu duniani.

Katika kipindi ambacho taasisi za elimu ya juu zinakabiliana na changamoto na fursa zinazotokana na AI, hatua ya UDSM kuingia katika mazungumzo na Harvard inaonekana kama mkakati wa mapema wa kuhakikisha Tanzania haiwi nyuma katika mapinduzi ya teknolojia.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Kikwete alisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi na yenye uwajibikaji ya AI, akibainisha kuwa teknolojia hiyo inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuboresha ubora wa elimu na utafiti iwapo itasimamiwa vyema.

Kwa upande wa Harvard, majadiliano yalihusisha viongozi na wataalamu waandamizi, akiwemo Mkuu wa Harvard Kennedy School, Prof. Jeremy M. Weinstein, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Maendeleo ya Kimataifa (CID), Dkt. Fatema Sumar.

Aidha, timu ya wataalamu wa AI kutoka Harvard ilishiriki majadiliano hayo, wakiongozwa na Prof. Sharad Goel, akishirikiana na Dkt. Dan Levy na Dkt. Teddy Svoronos—wote wakiwa na uzoefu mkubwa katika matumizi ya AI katika sera za umma na uchambuzi wa data.

Ushirikiano huu unatarajiwa kufungua ukurasa mpya katika sekta ya elimu ya juu nchini, kwa kuunganisha utaalamu wa ndani na uzoefu wa kimataifa katika matumizi ya teknolojia ya kisasa.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...